SERIKALI YAIPA TANROADS MWANZA BIL 58.27 KUJENGA DARAJA LA SIMIYU NA DARAJA LA SUKUMA
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 58.288 kwa ajili ya kujenga daraja la Simiyu na daraja la Sukuma mkoani Mwanza.
Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya ukaguzi katika daraja la Simiyu na Sukuma iliyofanywa na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS mkoa wa Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose pamoja na wataalamu mbalimbali kujionea hatua zilizofikiwa baada ya serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo
Mhandisi Ambrose amesema kuwa Mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Simiyu pamoja na Barabara unganishi ulitiwa saini kati ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkandarasi M/s China Civil Engineering Construction Corporation kutoka nchini China tarehe 6 Julai, 2023 akisimamiwa na Mhandisi Mshauri na Msimamizi kutoka kitengo cha TANROADS - (TECU) mkoa wa Mwanza.
"Muda wa utekelezaji wa mradi huo ulioanza kazi ya ujenzi tarehe 30 Octoba 2023 utakuwa ni miezi 18 kwa gharama ya shilingi Bil 48.788" Amekaririwa Mhandisi Ambrose
Akiwa katika daraja la Sukuma, Mhandisi Ambrose amesema kuwa Mkataba wa Ujenzi wa Daraja la hilo la Sukuma lenye urefu wa mita 70 pamoja na Barabara unganishi ulitiwa saini kati ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkandarasi Mumangi Constuction Co. Ltd.
Amesema kuwa Ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa Mita 70 pamoja na Barabara unganishi ambao unajengwa na TANROADS pia una Mhandisi Mshauri na Msimamizi kutoka kampuni ya M/s Advance Engineering Solutions Ltd chini ya mkandarasi M/s Mumangi Constuction Co. Ltd.
Mhandisi Ambrose ameongeza kuwa mkataba huo ulisainiwa tarehe 17 Disemba 2023 na kazi ya ujenzi ilianza tarehe 5 Machi 2024 ambapo muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 12 unatarajiwa kumalizika tarehe 4 machi 2025 kwa gharama ya Shilingi Bil 9.482 (bila VAT).
Mhandisi Paschal Amrose ambaye ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Mwanza amesema kuwa katika daraja la Sukuma kwa sasa Mkandarasi anaendelea na kazi ya kuchimba msingi wa daraja na ujenzi wa ofisi za mhandisi mshauri, pamoja na zoezi la ulipaji fidia kwa wenye maeneo yaliyoathirika na mradi.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/UOlShTb
No comments