Mabadiliko ya sheria ya sukari yatawakomboa Watanzania
Kufuatia upotoshaji unaoendelea kutolewa na baadhi ya watu wasiokuwa na ufahamu juu ya sheria mpya ya sukari, Bodi ya Sukari Tanzania imesema kupitishwa kwa sheria hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaenda kutowesha mfumuko wa bei ili isimuumize mwananchi, upatikanaji wa uhakika, uwazi katika usambazaji wake pamoja na ufanisi kwenye viwanda vya sukari nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache baada ya baadhi ya wadau wa sekta ya sukari kuelezea sakata hilo bila kuwa na taarifa za kutosha hali iliyoibua sintofahamu kwenye sekta hiyo nyeti nchini.
“Baadhi ya watu wanaoelezea suala la sukari hawana taarifa za kutosha, hivyo ni jukumu letu Bodi kutoka hadharani pamoja na mambo mengine, kutoa picha kamili ya namna gani Watanzania wanaenda kupata ahueni kubwa baada ya serikali kufanya mabadiliko katika sheria ya sukari nchini,”Alisema Profesa Bengesi.
Baadhi ya hoja zilizofafanuliwa na Bodi ya Sukari Tanzania ni pamoja na uhaba wa sukari, malalamiko ya utoaji wa vibali na mbinu zinazoenda kutumika kwa lengo la kuhakikisha uhaba wa sukari nchini unaenda kuwa historia.
No comments