Breaking News

JAPAN YAONGEZA SH. BILIONI 8.9 UKARABATI WA BANDARI YA KIGOMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa, wakisaini mkataba wa Marekebisho ya msaada wa nyongeza ya Yen za Japan milioni 548 sawa na shilingi bilioni 8.9 na kufanya jumla ya msaada kuwa shilingi bilioni 53.35, baada ya awali kutolewa shilingi bilioni 44.42 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma, hafla iliyofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Tanzania, Bw. Hitoshi Ara, wakionesha mkataba wa Marekebisho ya msaada wa nyongeza ya Yen za Japan milioni 548 sawa na shilingi bilioni 8.9 na kufanya jumla ya msaada kuwa shilingi bilioni 53.35 baada ya awali kutolewa shilingi bilioni 44.42 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma, hafla iliyofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Tanzania imepokea msaada wa nyongeza wa Yen za Japan milioni 548 sawa na shilingi bilioni 8.9 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma baada ya marekebisho ya mikataba miwili ya msaada kati ya Tanzania, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan na Ubalozi wa Japan.

 

Mikataba ya marekebisho ya msaada imesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Tanzania, Bw. Hitoshi Ara, kwa niaba ya Japan.

 

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa marekebisho ya mikataba hiyo, Dkt. Mwamba alisema kuwa, awali Serikali ya Japan kupitia mikataba iliyosainiwa Februari 4, 2022 ilitoa msaada wa Yen za Japan bilioni 2.73 sawa na shilingi bilioni 44.42 kwa ajili ya ukarabati wa Bandari hiyo.

 

Alisema jumla ya msaada uliotolewa na Serikali ya Japan unakuwa Yen za Japan bilioni 3.27 sawa na shilingi bilioni 53.35, ambapo fedha zilizoongezwa zinalenga kuziba pengo lililotokana na kuporomoka kwa thamani ya Yen za Japan na shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.


No comments