Breaking News

WANA-GDSS WAJENGEWA UWEZO JUU YA ULINZI WA MTOTO KISHERIA, USAWA WA KIJINSIA NA NAMNA YA KURIPOTI TAARIFA ZA UVUNJWAJI WA HAKI ZA MTOTO


Na mwandishi wetu, Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa, Serikali kuu hutoa majukumu kwa serikali za mitaa katika kulinda na kutetea maslahi ya mtoto ili kuhakikisha kuwa analelewa katika mazingira stahiki na kwa maadili ya jamii.

Vilevile maafisa ustawi wa jamii wana wajibu wa kushirikiana na serikali za mitaa kutoa ushauri na elimu kwa wazazi, walezi, ndugu na jamii kwa ujumla juu ya ustawi wa mtoto.

Hayo yamesemwa kwa nyakati Juni 19, 2024 jijini Dar es Salaam na Nasra Mrisho pamoja Wenseslaus Kidakule ambao ni wawazesheaji kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwenye Semina za Jinsia na Maendeleo iliyofanyika katika ofisi za TGNP Mabibo ambapo mada kuu kwa hii leo ilikuwa ikiangazia kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu (2024) inayosema Elimu Jumuishi kwa Watoto, Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.

Wawili hao, wametilia mkazo suala la ulinzi wa kisheria wa makazi ya mtoto ambapo wamesema, watoto wana haki zote za kufurahia na kufaidika na mali za wazazi wake pasi na kumfanyia mtoto ukatili au unyama wa aina yoyote ile utakaoathiri akili au maumbile yake.

Kuhusu suala la usawa wa kijinsia, wawezeshaji hao wameeleza kuwa, sheria inakataa ubaguzi wa aina yoyote ile kwa mtoto iwe ni rangi, dini, ukimbizi, ulemavu au ubaguzi mwingine wowote na kwamba watoto wote wanapaswa kuchukuliwa kwa mizani sawa.

Vilevile wameikumbusha jamii kuwa, ina wajibu wa moja kwa moja wa kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa juu ya uvunjwaji wa sheria kuhusu watoto utakaofanywa na mzazi, mlezi, ndugu au mtu yeyote yule.

Akichangia mada katika semina hiyo, mwanaisaikolojia Sylvia Sostenes amewasihi na kuwakumbusha wazazi kukaa na watoto wao na kuwaeleza ni kwa lengo gani wanawapeleka watoto wao shule, kitu ambacho ni kinyume na sasa akibaini watoto wengi wanakwenda shule kwa kuwa kuna utamaduni wa kwenda shule kusoma au mtoto kuona watoto wa jirani wakienda shule lakini si kuwa na utambuzi wa lengo husika.

"Kama tukikaa nyumbani na kuongea na watoto wetu na kuwaeleza kuwa ni kwa sababu gani wako shule itasaidia sana na pia itawafanya watoto wenyewe waweke bidii kutoka mioyoni mwao katika masomo yao" alisema Sylvia

Kando na hilo, amewataka wanaharakati wa jinsia kuendelea kupaza sauti na kupinga kila aina ya unyanyasaji ambapo kwa mazingira mjini wanafunzi wengi wananyanyaswa katika vyombo vya usafiri.

"Tukatae hilo na kupaza sauti tukiwa ndani ya vyombo vya usafiri na ikiwezekana tukutane na makondakta wa vyombo vya usafiri ili kuongea nao na kuwapa elimu, watoto wanafanyiwa unyanyasaji lakini watu wazima wapo ndani ya gari na wako kimya" amehoji Sylvia

Pia amezitaja baadhi ya changamoto ambazo zinakwamisha jitihada za watoto kupata elimu hususan maeneo ya pembezoni mwa miji na vijijini kuwa ni pamoja na uwezo mdogo kukidhi mahitaji ya msingi ya mwanafunzi.

Kufuatia hilo ameiomba serikali, kuweka wazi kiwango cha ruzuku inayotolewa kwa kila mwanafunzi ili iweze kutumika katika mahitaji ya kimsingi kama ununuzi wa sare za shule.

Kenedy Angeliter, ambaye ni mshiriki katika semina hiyo, ametoa rai kwa serikali kuhakika elimu inayotolewa na kuhakikisha inakuwa bora na si bora elimu pamoja na kusimamia sera ya elimu iliyopo ili kuleta mtazamo mpya wa fikra na kuachana na mtazamo wa awali wa kusoma kwa lengo la kujipatia ajira pekee.

Angeliter ameongeza kuwa, imekuwa ni utamaduni kwa sasa kwa wahitimu wa elimu mbalimbali kutembea na bahasha zenye wasifu wao kwa lengo la kutafuta fursa za ajira.

"Inabidi tubadilishe mitazamo ya wanafunzi wetu wafahamu kabisa kwamba pindi wanapohitinu wanapaswa kwenda kujiajiri"

Semina za Jinsia na Maendeleo hufanyika kila siku ya Jumatano na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo, wanahabari, wanasaiokolojia, wanaharakati na wanajamii kwa ujumla ambapo kwa pamoja huadili kuhusu mada mbalimbali zenye mrengo wa kijinsia na maendeleo.


from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/WP8K57D

No comments