TPDC YAHAMASISHA ULINZI NA USALAMA WA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA MTAA WA ULONGONI A, DAR ES SALAAM
Juni 8, 2024
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni Tanzu ya GASCO limeendea kuelimisha Umma juu ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya bomba la gesi kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara. Elimu ya mara kwa mara imekuwa na matokeo chanya kwani ulinzi wa miundombinu ya gesi asilia umeendelea kuimarika hali inayopeleka miundombinu hiyo kuwa salama nyakati zote.
Katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Ulongoni A, sambamba na mambo mengine elimu ya ulinzi na usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia ilitolewa. Aidha, Katika kuhakikisha miundombinu inakuwa salama ajenda ya ulinzi na usalama imekuwa ya kudumu kwenye Mitaa na Vijiji vyote vinavyopitiwa na miundombinu hiyo kuanzia Mtwara hadi Dar es salaam.
Dikson Kibala ambaye ni afisa ulinzi na usalama wa miundombinu ya bomba la gesi asilia alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mtaa wa Ulongoni A katika kuimarisha ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za kiusalama pamoja na kushirikiana kukomesha shughuli zote za kibinadamu ndani ya Mkuza wa gesi asilia kama kuchimba mchanga/kokoto, ujenzi n.k.
"Tunapongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Mtaa wa Ulongozi A kwa kuimarisha ulinzi pamoja na kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na TPDC/GASCO kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na usafi wa Mkuza", aliongeza Kibala
Afisa Ulinzi na Usalama wa miundimbinu ya gesi asilia Ndg Dickson Kibala akitoa elimu ya ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Mtaa wa Ulongoni A- Ndg Abdulrahim Munisi alipongeza jitihada zinazofanywa na TPDC kwenye kutoa elimu pamoja na kuinua huduma mbalimbali za kijamii kwenye mitaa inayopitiwa na midombinu ya bomba la gesi ikiwemo mtaa wa Ulongoni A.
"TPDC/GASCO mmekua wadau wa mfano kwenye kushirikiana na jamii, tunashukuru kwa kutupatia fedha za kujenga ofisi nzuri ya Mtaa tena ya kisasa ambayo kwa sasa imekamilika na inatumika kuhudumia wananchi, mtaa wetu utaendelea kutoa ushirikiano katika kulinda miundombinu ya bomba la gesi asilia", aliongea Mwenyekiti Munisi.
Kwa upande wake, Mhe Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto Mhe. Lucas Lutainurwa alitoa shukrani kwa uongozi wa TPDC/GASCO kwa kuendelea kuinua huduma za kijamii ikiwemo sekta ya elimu kwenye kata ya Gongo la mboto. Aidha alitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia juhudi za serikali kwenye kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama Maji, Elimu na Afya.
Diwani wa kata ya Gongo la Mboto Mhe Lutainurwa akiongea wakati wa mkutano na wanachi wa Mtaa wa Ulongoni A-Dar es salaam
"Mwaka 2022/2023 tulipokea Tsh 69,000,000 kutoka TPDC/GASCO kwa ajili ya Ujenzi wa Bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mzambarauni, ni jambo kubwa na la kujivunia kwani ujenzi wa Bweni ulikamilika na tayari linatumika", aliongea Lutainurwa.
#TPDC TUNAWEZESHA.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/N2PVUCi
No comments