TANESCO KUOKOA BILIONI 30 KILA MWAKA MKOA WA KAGERA UTAKAPOINGIA KWENYE GRIDI YA TAIFA
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litaokoa kiasi cha Shilingi bilioni 30 kila mwaka baada ya Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka kukamilika jambo litakaloimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kagera kwa kuwezesha Wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba vijijini na Manispaa ya Bukoba kuunganishwa katika Gridi ya taifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Gissima Nyamo – Hanga wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba na Mhandisi Mshauri (Shaker Consultancy Group) kutoka nchini Misri ikishirikiana na Kampuni ya usimamizi miradi ya umeme ya Saudi Arabia (PDC) leo Juni 12, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Shirika Masaki, Dar es salaam kwa ajili ya kuandaa nyaraka za manunuzi ya wakandarasi wa ujenzi pamoja na usimamizi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovoti (220) ya Benaco hadi Kyaka Mkoani Kagera.
“Kwa sasa matumizi kwa mwezi ya kununua umeme kutoka Uganda unaotumika mkoa wa Kagera ni karibu shilingi bilioni 2.6 ambayo ni karibu bilioni 30 kwa mwaka. Pindi mkoa wa Kagera utakapounganishwa kwenye gridi ya taifa, kiwango hicho cha fedha kitaokolewa na kuwezesha fedha hiyo kutumika kuboresha miundombinu yetu ya umeme katika maeneo mengine”, amesema Mha. Nyamo – Hanga
Ameongeza kuwa, ujenzi wa njia hiyo ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kagera ambapo Wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba vijijini na Manispaa ya Bukoba zitaunganishwa katika Gridi ya taifa ambazo zimekuwa zikipokea umeme kiasi cha Megawati 21 kutoka nchini Uganda kupitia kampuni ya kusafirisha umeme ya (UETCL).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shaker Consultancy Group Dr. Ismail Shaker amesema kuwa kwa zaidi ya miaka nane wamekuwa wakifanya kazi na nchi za Afrika na Tanzania ni nchi ya kipekee wanayopenda kushirikiana nayo katika sekta ya umeme.
“Napenda kuishukuru TANESCO pamoja na Mkurugenzi mtendaji kwa kutuamini na nichukue nafasi hii kumhakikishia na kuwahakikishia wote hapa ya kuwa tutafanya kila tunaloweza kufikia matarajio. Tunafahamu TANESCO inataka kuifanya nchi hii kuwa kinara kwenye uzalishaji wa umeme na tunafuraha kuwa sehemu ya timu hii”, amesema Dr. Shaker
Ujenzi wa mradi huu utagharimu kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 135. 4 ukihusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme ya umbali wa kilometa 166.17 kutoka Benaco mpaka Kyaka,ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha Benaco na kukiongezea uwezo wa kituo cha kupoza umeme Kyaka kilichopo sasa.
Mradi huu utagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kiasi cha Shilingi za kitanzania Bilioni 6.2 wadau wa maendeleo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Saudi (SFD) Dola za Marekani Milioni 13,Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi Dola za Marekani Milioni 30 na Mfuko wa Maendeleo ya Kimataifa wa OPEC ambao utachangia kiasi cha Dola milioni 60 za Marekani.
Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huu anatarajiwa kupatikana mwezi Disemba 2024 na utekelezaji wa mradi utakamilika Disemba 2026.
No comments