Serikali yaondoa hofu ya Umeme kutofika vitongoji vyote nchini
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata umeme ambapo mpaka sasa vitongoji 33,000 vimesambaziwa umeme kati ya vitongoji zaidi ya 60,000.
Mhe. Kapinga amesema hayo tarehe 21 Juni 2024, Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu maswali mbalimbali ya Wabunge katika kipindi cha Maswali na Majibu.
Kapinga amesema kutokana na suala la maendeleo kuwa ni hatua, Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Mhe. Edwin Swale kuhusu mpango wa Serikali kupeleka umeme wa REA kwenye Vitongoji, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Lupembe lina vitongoji 227 ambapo vitongoji 118 vimekwishapatiwa umeme na vitongoji 109 vilivyobaki Serikali pia itavipelekea umeme.
Ameongeza kuwa, vitongoji 19 kati ya hivyo vitapatiwa umeme kupitia mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu. Vile Vile, vitongoji 15 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kila Jimbo, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Aidha, Vitongoji 75 vitapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa “Hamlet Electrification Project” ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/25 kulingana na upatikanaji wa fedha.
Akizungumzia Kijiji cha Madeke na maeneo ya uwekezaji katika mji wa Njombe kupatiwa umeme Mhe. Kapinga amesema Serikali itafuatilia ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini mkubwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi.
Akijibu swali la Mhe. Yahaya Masare, Mbunge Jimbo la Manyoni Magharibi kuhusu kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya Halmashauri ya Itigi, Mhe. Kapinga amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo, ikiwa ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema kupitia mwaka wa fedha unaokuja wa 2024/25, Serikali imetenga fedha za kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000.
Akijibu swali la Mhe. Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu aliyetaka kufahamu ni lini vitongoji ambavyo havina umeme katika Mkoa wa Simiyu vitapata umeme, Mhe. Kapinga amesema ipo miradi inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa ujazilizi na kuongeza kuwa, kutokana na Serikali kuona umuhimu wa umeme kwa wananchi imebuni miradi mbalimbali itakayotimiza dhamira ya Serikali ya kila mwananchi kupata huduma ya umeme.
Akijibu swali la Mhe. Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum ambaye alitaka kufahamu kuhusu umeme kufika kwenye baadhi ya Kata ambazo zipo vijijini katika Jimbo la Bunda mjini kati ya kata 14 kata 7 zipo Vijijini, Mhe. Kapinga amesema kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imefanya utaratibu wa kuhakikisha mitaa ya Bunda mjini ambayo haina umeme inapata umeme na itaendelea kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji.
Aidha, aikibu swali la nyongeza kutoka kwa Mhe. Daimu Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kuhusu lini Mkandarasi anayetekeleza miradi ya ujazilizi ataanza kazi, Mhe. Kapinga amesema kutokana na kuelekea kukamilika kwa miradi ya umeme vijijini, hivi karibuni inaanza miradi ya ujazilizi katika Vitongoji vya jimbo la Tunduru Kusini.
Aidha, kuhusiana na Vijiji vingine kurukwa kupatiwa umeme Mhe. Kapinga Wabunge kuwa maendeleo ni hatua hivyo maeneo yote yatafikiwa na umeme kwa awamu.
Akijibu swali la Mbunge wa Kilosa. Mhe. Palamagamba Kabudi aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme eneo la Dumila, Kilosa, Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila yenye urefu wa kilomita 66 pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Magole – Dumila kupitia mpango wa Gridi Imara awamu ya pili unaotarajia kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwaka 2026.
Kuhusu Serikali kuimarisha Ofisi ya TANESCO Dumila ili iweze kutoa huduma bora Mhe. Kapinga amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanachi ili waendelee kupata umeme wa uhakika.
Ameongeza kuwa, maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ni kuhakikisha wafanyakazi wa TANESCO wanafanya kazi kwa weledi na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme katika maeneo yote Tanzania.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Mhe. Benaya Kapinga kuhusu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kapinga amesema mradi wa kituo hicho upo katika hatua za utekelezaji na unatakiwa kuanza awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukamilika.
Ameongeza kuwa, Serikali itausimamia mradi huo kwa weledi na nguvu ili uweze kukamilika na kuongeza kuwa Serikali imeboresha njia ya umeme ambayo inapeleka umeme kutoka Songea hadi Mbinga na laini za Mbinga Vijijini.
Vilevile, kuhusu swali la Mhandisi Mhe. Samweli Ayuma, Mbunge wa Hanang ambaye alitaka kufahamu ni lini kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Hanang kitajengwa, Mhe. Kapinga amesema kipo katika awamu ya pili ya utekelezaji.
No comments