Breaking News

Serikali: Mkopo wa dola Bilioni 2.5 hauna mashari ya kuweka rehani Bahari na Madini.



Mafanikio ziara ya Rais Dkt. Samia nchini Jamhuri ya Korea yatajwa

Na ABRAHAM NTAMBARA NA TUNU BASHEMELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo amesema  mkopo wa dola Bilioni 2.5 ambao Tanzania imeupata kutoka Korea hauna masharti ya kuweka rehani rasilimali za Tanzania kwa kuwapa Wakorea bahari na madini kama inavyosambazwa mitandaoni.

Prof. Mkumbo amebainisha hayo jana akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu, Dar es Salaam kuhusu masuala ya Uwekezaji wakati wa Ziara Rasmi ya Kiserikali aliyofanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia Mei 31 hadi Juni 6, 2024, Jijini Seoul, Jamhuri ya Korea.



Alieleza kuwa mkopo huo una faida kubwa kwa Nchi na kwamba huo sio mkopo wa kwanza kwa Tanzania kupokea kutoka Mataifa mbalimbali Duniani na hakuna mkopo hata mmoja ambao ulipokewa kwa masharti ya kuweka rehani Rasilimali za nchi.

“Kuna hili lililosambaa kwenye mitandao kwamba tumechukua mkopo wa dola bilioni 2.5 kwa kubadilishana na kuwagawia bahari na madini yetu, kwanza huu sio mkopo wa kwanza ambao tunauopokea kutoka Mataifa mbalimbali Duniani na hakuna mkopo hata mmoja ambao tumewahi kuupokea kwa maana ya kuweka rehani rasilimali zetu mojawapo hasa rasilimali za asili, haupo," alisema Prof. Mkumbo na kuongeza,

“Pili sio mkopo wa kwanza kupokea kutoka Korea huu ni mpango wa pili tulikopa bilioni 1 na mwaka huu bilioni 2 ukijumlisha na ile tuliyoibeba inakuwa bilion 2.5, kwanza kukopa ni muhimu kwasababu ni moja ya nyenzo za kujenga uchumi wetu, kujenga uwezo wa Serikali kutoa huduma kwa Wananchi wake, muhimu tu ni kwamba unakopa kupeleka wapi na kwa masharti gani,”.

Prof. Mkumbo alibainisha kwamba, kipaumbele cha Tanzania ni kuchukua mikopo yenye masharti nafuu na kwenda kuwekeza kwenye Sekta za uzalishaji.

"Hatukopi kwenda kununua magari na kulipana mishahara, huu mkopo ni wa miaka 40 na riba yake ni asilimia 0.01 na tunaanza kulipa mwaka wa 26, kwahiyo hayo masharti yaliyosemwa hayapo na tumefafanua, Balozi amefafanua," alisisitiza Prof. Mkumbo.



Kuhusu maeneo ya kipaumbele kwenye ushirikiano wa kiuwekezaji na kibiashara baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, Prof. Mkumbo alisema ni meneo matatu ambayo ni Mosi, uwekezaji kwenye Sekta ya kilimo, Pili, uwekezaji kwenye Sekta ya Madini ya Kimkakati na Tatu, kukuza biashara kati ya Tanzania na Korea kwa kuongeza thamani ya madini, mifugo na kilimo.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Nape Nnauye, akizungumza kuhusu Tanzania ililojifunza kutoka Korea kwenye sekta ya Teknolojia, amesema mchakato wa Tanzania kuwa na satelaiti yake yenyewe unaendelea vizuri na kusema endapo mchakato utakamilika satelaiti hiyo itasaidia kuboresha huduma za mawasiliano hadi vijijini.

Alisema, nchi ya Korea imepiga hatua kubwa kwenye miundumbinu ambapo kwa Tanzania, Serikali inaendela na uwekezahi na kwamba uwekezaji huo ni gharama.


"Kingine wenzetu wanazalisha smart device kwa maana ya simu janja, sisi kwetu tuna changamoto ya kusambaa kwa vifaa hivyo kwasababu ni ghali, moja ya eneo ambalo tumezungumza kwa kina ni kuona namna ambavyo tunaweza kushirikiana nao tukazalisha hapa kwetu kwa maana ya kuviunganisha vifaa ambavyo vitakuwa kwa bei nafuu ili Watanzania waweze kuvimudu,” alisema Nape na kubainisha kuwa,

“Najua swali kubwa hapa ni kwamba miundombinu vijijini ikoje, mtakumbuka bajeti yetu iliyopita tumetangaza mchakato wa kuwa na satelaiti yetu kama Nchi, mchakato huo unaendelea vizuri, zipo Timu zimeenda Duniani, Katibu Mkuu na Timu yake walikuwa China, wengine wataenda Marekani na kwingine , baada ya pale pamoja na miundombinu mingine ambayo tunaendelea lakini hili la kuwa na satelaiti yetu kama Nchi linaendelea vizuri na changamoto hizi zitapungua,”.

Hata hivyo ili tuweze kupiga hatua ya maendeleo zaidi ni lazima tujenge utamaduni wa kufanya kazi badala ya utamaduni wa Watu kushinda mtandaoni masaa 24 ampabo alisisitiza utamaduni huo upigwe vita.

"Vinginevyo hatuwezi kutoka, na ni kupitia kazi, Watu wasifikiri kuna Mjomba atakuja mahali akuletee maendeleo ya maisha yako,” alieleza Nape.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akitaja changamoto zinazoikabili Tanzania katika biashara na mataifa mengine ikiwemo Korea ni bidhaa zinazozalishwa kukosa viwango vya ubora vinavyokidhi kimataifa, bidhaa kukosa uasili na kukosekana kwa uendelevu wa biashara kutokana na uchache wa bidhaa zinazozalishwa.

Hivyo ili kuweza kufanya vizuri kwa bidhaa za Tanzania ni lazima zizalishwe kwa ubora unaokidhi viwango vya kimataifa, bidhaa ziwe na uasili wake pamoja na kuhimiza uwekezaji kwenye uzalishaji wa bidhaa ili ziwepo za kutosha.

Awali Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus akieleza muhtasari wa yaliyofanyika wakati wa zira hiyo, alisema Rais Dkt. Samia alitembelea Kituo cha Kubadiliana Maarifa ya Kidunia na Maendeleo (GKED), alishuhudia utiaji saini wa mkataba mmoja, Hati za Makubaliano (MOU) mbili na Tamko la pamoja la kuanzisha mkataba wa ushirikiano wa uchumi (EPA).

Aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia alitunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima kwenye Sekta ya Anga (Honoris Cause) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korean Aerospace University), alikutana na kuzungumza na Mwimbaji Maarufu wa Muziki wa Jamhuri ya kaorea Cho Yong-pil, jijini Seoul, alishiriki Mkutano wa Korea na Afrika, Kintex nje ya kidogo ya Jiji la Seoul.

Kadhalika alishiriki Mkutano wa Jukwaa la Miundombinu kati ya Korea na Afrika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea na mwisho alizungumza na (Diaspora) Watanzania wanaoishi katika nchi ya Jamhuri ya Korea jijini Seoul.

No comments