Rais Samia amuagiza msajili wa hazina kufuatilia hesabu za mashirika yote kwenye mfumo
Na: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu kuhakikisha anaweza kuona hesabu za mashirika yote anayoyasimamia ikiwa ni pamoja na makusanyo na matumizi yao.
Rais Samia ameyasema hayo katika hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika na Taasisi za Umma, iliyofanyika Juni 11, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu kuona kile kinachoingia na kinachotoka kwani hiyo itasaidia kufahamu uwezo wa mashirika hayo kiuchumi na namna yatakavyoweza kujisimamia yenyewe.
“Yapo mashirika ambayo yanaweza kabisa kusimama yenyewe, mfano Ngorongoro inaweza kusimama yenyewe kwa sababu tumetengeneza mazingira watalii wanakuja mpaka wanacheua sasa kwanini isisimame, kwanini Tanapa isisimame yaani hakuna sababu.
“Naziagiza bodi za mashirika kubadilika na kuyasimamia kikamilifu hakuna sababu ya mashirika na taasisi zote za Serikali katika kutekeleza hili. Hakuna sababu ya mashirika haya yasiweze kujisimamia yenyewe” amesema Mhe Rais.
Aidha ameongeza kuwa ameridhishwa na uwepo wa ushindani wa wajumbe wa bodi katika kupata nafasi hizo na kwamba hatua hiyo itapelekea kuwapata wajumbe wa bodi wenye weledi na wanaofahamu vizuri mambo yanayoendelea ndani ya mashirika.
“Jambo zuri ni kwamba mjumbe wa bodi sasa watashindana kuitaka nafasi hiyo katika Shirika au Taasisi unayoitaka itabakia nafasi yangu ya mimi kuchagua Mwenyekiti” ameongeza Rais Samia.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema kuwa Ofisi yake ipo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti taarifa za kiutendaji na wakuu wa Taasisi kwa kumwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati kwa mamlaka za uteuzi.
Aidha, amesema Ofisi hiyo imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika vilivyoingizwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina.
“Vigezo hivi vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi, na tutaendelea kuboresha vigezo hivi mara kwa mara, kwa kutegemea mrejesho kutoka taasisi zetu hizi ambao ndio wadau wetu” amesema Mchechu.
Mchechu ameongeza kuwa, pia Ofisi hiyo imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia kwenye sekta nyeti za uchumi.
“Kwenye sekta ya madini kumekuwa na mazungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini. Tumeweza kuongeza hisa za Serikali katika baadhi ya Kampuni, Mathalani tumeongeza hisa za Serikali katika Kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo” ameongeza Mchechu.
Sambamba na hilo pia wamefanikiwa kukamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na kampuni ya NMB, NBC na MCCL, ambapo kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza kupata faida mwaka huu na kutoa gawio kwa wanahisa mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10.
Kuhusu gawio, Mchechu ametoa Rai kwa Mashirika ambayo yanadaiwa kuhakikisha wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha.
No comments