Mwafaka wa kitaifa ni muhimu katika kupata Dira Bora ya 2050 - Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
MWAFAKA WA KITAIFA NI MUHIMU KATIKA KUPATA DIRA BORA YA 2050 – MAELEZO YA NDUGU ZITTO KABWE, KIONGOZI WA CHAMA WA ZAMANI WA ACT WAZALENDO KATIKA KONGAMANO LA DIRA YA TAIFA 2050
DIRA 2025: Dira ya Taifa ya 2025 ilieleza
yafuatayo “Mtanzania
atakayezaliwa leo atakuwa
ni mtu mzima, atakuwa
amejiunga na kundi la wafanyakazi, na labda atakuwa
ameanza kuwa mzazi ifikapo mwaka 2025. Hali kadhalika,
Mtanzania ambaye ameanza kufanya kazi hivi karibuni atakuwa anajiandaa kustaafu ifikapo mwaka
2025. Je! ni jamii ya aina
gani itakayokuwa imejengeka ifikapo mwaka 2025?
Kinachotarajiwa
ni kuwa jamii ambayo Watanzania hawa watakuwa wakiishi wakati huo itakuwa ni yenye
maendeleo ya kuridhisha na maisha bora. Umasikini uliokithiri utaondoka na kubaki
kuwa jambo la kihistoria. Kwa maneno mengine,
inategemewa kwamba Watanzania watakuwa wamejikomboa
kutoka katika kundi la nchi maskini na kuweza kuingia
katika kundi la nchi zenye viwango vya kati vya mapato na hali bora ya maisha ifikapo
mwaka 2025. Uchumi utakuwa
umebadilika kutoka uchumi
unaotegemea kilimo chenye
tija ndogo na badala yake kuwa na uchumi wenye kuongozwa
na sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa chenye
tija kubwa na kinachohusiana kwa karibu na maendeleo ya viwanda
na sekta za huduma mijini
na vijijini”. Mwisho wa kunukuu.
Mawali muhimu la kujiuliza ni; Je Malengo hayo ya Dira ya 2025 yamefikiwa? Je umasikini uliokithiri umeondoka? Je umoja na mshikamano wa kitaifa uko katika hali gani sasa? Je hali ya uchumi na maendeleo ya nchi ikoje?
Ili kupata majibu ya maswali hayo,
ningependekeza tufanye yafuatayo;
1. TUTATHMINI TULIKOTOKA: Lazima tuwe na mjadala wa ukweli (Honest Conversation) miongoni mwetu Watanzania bila ubaguzi
wowote kuhusu Miaka
25 na hata 60 iliyopita. Je tulikuwa na mwafaka wa kitaifa kuhusu DIRA? Je tulikuwa na nidhamu
ya
kutosha kutekeleza DIRA
2025? Kwanini ilichukua Miaka 10 kuanza kutekeleza DIRA?
Ilikuwa Dira Shirikishi? Kwa miaka
hii 25 Vyama vya siasa viliunda Ilani zao kwa kufuata Dira hiyo?
Wanaotuongoza walifanya maamuzi
kwa kuzingatia Dira? Tuwe tayari kukubali
matobo na kuweka mikakati ya kuziba matobo hayo. Na wasilisho la Profesa Shivji kwa kiasi
limejikita kwenye pendekezo
hili, natarajia siku za mbeleni tutakuwa na makongamano ya ya kujadili masuala
makhsus ya kila sekta, kama Siasa, Uchumi,
hali ya jamii nk, ili kuwa na tathmini ya kina
juu ya miaka 25 ya utekelezaji wa Dira tunayoitekeleza sasa.
2. MWAFAKA WA KITAIFA: Baada ya tathmini ya hapo juu (HONEST CONVERSATION), tujenge MWAFAKA WA KITAIFA kuhusu tunapotaka kuipeleka Tanzania. Lazima,
na ni muhimu kwa watu wenye kufanya maamuzi na wenye ushawishi wa kimaamuzi (Viongozi wa Serikali, Watumishi
wa Serikali, Wanasiasa
wa Upinzani, Wafanyabiashara, Watendaji wa Mashirika ya Umma, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi,
Wafanyakazi, Wanasanaa, Wanafunzi, nk) – Mimi naiita Mass bargain, kukubaliana mwafaka wa kitaifa
(commitment to growth and development).
3. DIRA YA WOTE, DIRA YA TAIFA: Mwafaka wa Kitaifa utazalisha Dira ya 2050 yenye mchango wa Watanzania wote, juu ya namna wanavyotaka Tanzania ya mwaka 2050 iwe, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Dira ya namna hii itakuwa na uhalali wa kisiasa na kijamii, itatambulika na umma, na utakuwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anafanya juhudi kwa nafasi yake ili Dira husika ifikiwe. Hii itakuwa ni DIRA YA WOTE, DIRA YA TAIFA.
Baada ya Utangulizi huo, yafuatayo ni mambo muhimu ambayo tunapaswa kuyazingatia kuelekea Dira 2050;
PATO LA TAIFA NA PATO LA MTU MMOJA MMOJA (GDP NA
PER CAPITA): Tanzania ya Mwaka 2050 itakuwa na Watu takribani milioni 130, zaidi ya mara mbili ya watu wote walioko
sasa. Tukiweka lengo la kuwa na Pato la mtu mmoja mmoja la USD 3,500 kwa mwaka ifikapo
2050 (zaidi ya mara mbili
ya GDP/capita ya sasa ya USD 1200)
tunahitaji Uchumi
wa Tanzania uongezeke mara 6.5 hadi kufikia USD 455 Bilioni. NI jambo linalowezekana, kwani kati ya 2000 -
2022 GDP iliongezeka mara 5.8 kutoka USD 13 Bilioni
mpaka USD 75 Bilioni. Hivyo, kasi ya kukua kwa Uchumi
inapaswa kuwa Wastani wa 8% kwa mwaka kwa miaka 10 ya mwanzo (yaani
2026 – 2036), na kasi hiyo
isishuke 6% kwa miaka mingine 15 mpaka mwaka 2050. Dira ya 2050 inapaswa kulitazama
kwa kina jambo hili.
KILIMO: Kasi hiyo ya ukuaji
wa Uchumi itapaswa
kuongozwa na sekta ya
Kilimo, 6 - 8% kwa mwaka. Tunapaswa kuweka nguvu kubwa katika TIJA kwenye Kilimo, angalau tuongeze mavuno mara mbili (doubling) ya sasa katika
kila Ekari ya mazao
ya Kilimo. Nina mfano napenda kuutoa, wa zao la Pamba, ambapo ilhali
mkulima wa Tanzania
anapata kilo
250 - 300 kwa kila ekari ya Pamba, mkulima wa Benin anapata kilo 800 na mkulima wa Burkinafaso anapata kilo 1500. Hali ni mbaya zaidi kwenye Mahindi na Mpunga ambapo wakulima wetu wanapata gunia chache zaidi kutoka kila ekari 1!. Dira ya 2050 inapaswa kulitazama kwa kina jambo hili.
VIWANDA NA MADINI: Ni lazima tuongeze ajira kwa kuhakikisha
mnyororo wa viwanda vya kuongeza thamani ya
mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi unafungamanishwa na sekta
yetu ya kilimo. Ni lazima kuongeza tija ya mazao yetu ili yasiuzwe yakiwa ghafi. Zamani niliwahi kuandika
ningeanza na nini kati ya Reli ya SGR na Mgodi wetu wa Mchuchuma
na Liganga. Ni jambo zuri tumejenga Reli ya
SGR,
lakini zaidi ya 75% ya fedha zilizotumika kwenye ujenzi huo
zimekwenda nje ya nchi (Japan na Uturuki) kununua chuma na mataruma, ilhali chuma tunacho
mchuchuma na Liganga Njombe na Ruvuma, mabehewa ya SGR yamekuja, lakini makochi na viti havijatengenezwa
na mkonge wa Tanga wala Pamba ya
Simiyu, ama ngozi ya mifugo yetu, tumeendelea
kuuza ngozi ghafi, katani ghafi na pamba ghafi. Tuna hifadhi ya Dhahabu, Almasi na Shaba, na tuna Hifadhi
ya Madini Adimu Duniani (Rare Earth
Metals), tunafaidika vya kutosha? Tunaongeza Ajira Nchini? Dira ya 2050 inapaswa ilitazame hili.
AJIRA NA UMASIKINI: Watanzania wengi ni masikini na
wengi wao wanazunguka kwenye
mstari wa umasikini. Walio juu wakipata
Dhoruba (shock) kidogo wanadondoka, walio chini wakipata Msukumo
(boost) kidogo wanapanda. Wajibu wa Uongozi
ni kuwapandisha walio chini na kuwahami walio juu wasidondoke. Hifadhi ya Jamii kwa
wote ndio jawabu ya hilo.
Njia nzuri ya kuongeza watu kwenye hifadhi ya Jamii ni kuongeza
Ajira na Shughuli
za maendeleo. Kwa sasa uchumi wetu hauzalishi
Ajira za kutosha, vijana wengi hawana
ajira kabisa, na hawana mitaji
na mazingira wezeshi
ya kujiajiri, hivyo tunaongeza tu watu wanaoanguka kwenye lindi la umasikini. Dira ya 2050 lazima ishughulike na masuala ya ajira na umasikini wa watu wetu.
HIFADHI YA JAMII NA MITAJI: Tanzania inahitaji kujenga uwezo
wa ndani wa mitaji ili Sekta Binafsi ipate mitaji ya kuwekeza katika kukuza Uchumi. Uwezo
wetu wa ndani
wa kuweka akiba ni mdogo.
Uwiano wa Akiba na Pato la Taifa (Savings
- GDP ratio) ni chini ya 16%. Hivyo tunapaswa
kujenga mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii (social security) ili kujenga uwezo wa watu wetu
kuweka Akiba pamoja na kusaidia kuwatoa
watu wetu kwenye
umasikini. Uendeshaji wa miaka 25 sasa wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii una shida, Mafao na
Vikokotoo havichochei watu kuweka akiba
ya hifadhi ya jamii, mifuko yetu ya Bima ya Afya inakaribia kuanguka nk. Kwa nchi za wenzetu, mifuko ya Hifadhi
ya Jamii ndio chanzo kikuu cha mitaji ya mikopo kwa Serikali na Sekta binafsi, huko kote tunakokopa nyingi
ya fedha tunazokopeshwa zinatokana
na akiba za hifadhi ya jamii, tunao wajibu wa kuhakikisha tunajenga akiba
kubwa ya hifadhi ya jamii
ili kuwa na uhakika wa mitaji ya ndani. Dira ya 2050 inapaswa kulitazama kwa kina jambo
hili.
JIOGRAFIA NA BANDARI: Jiografia yetu pekee inaweza kuifanya Nchi yetu kuwa na mapato ya kigeni ya zaidi ya USD 12 Bilioni kwa mwaka na makusanyo ya kodi ya USD 10 Bilioni kila mwaka kutoka katika Forodha (Customs) peke yake. Tumezungukwa na DRC, Zambia, Uganda, Rwanda, Burundi na Malawi ambao wanatutegemea sisi kuifikia bahari. Hivyo tuboreshe ufanisi wa Bandari ili utumike kusaidia sekta nyengine kama Usafirishaji, Biashara na Uhifadhi ili kuhakikisha Jiografia yetu inatufaidisha zaidi. Dira ya 2050 inapaswa kulitazama kwa kina jambo hili.
UONGOZI NA SIASA: Juzi tumeona uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini, chama cha ANC kimeshindwa kupata
kura za kutosha (majority) kwa mara ya kwanza tangu 1994,
kitapaswa kuongoza na vyama vyengine,
na inawezekana kabisa kisiwe kwenye
uongozi miaka kadhaa mbele. Hapa kwetu CCM wanajiona
wao tu ndio wenye haki ya kuongoza,
hata pale wanapokataliwa kwa
kura na wananchi, na vyombo vya Dola vimetumika kusaidia CCM kusalia madarakani
hata pale walipokataliwa, tunayo
mifano ya Zanzibar tangu 1995, mfano wa karibuni zaidi ni uchaguzi
wa Serikali za Mitaa 2019
na Uchaguzi Mkuu wa 2020. Dira ya 2050 inapaswa
kuwekwa juu ya misingi
kuwa CCM inaweza kuondolewa madarakani, hivyo
nchi yetu inapaswa kuwa na uwezo
wa kuongozwa na chama
chochote kile ambacho wananchi watakichagua.
Tujenge uwiano na uwanja sawa wa kufanya siasa na kupata uongozi wa nchi, ili vyama vya siasa vibishanie mbinu
tu za kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 kupitia ilani.
NIHITIMISHE mchango wangu kwa kuainisha Mtanzania, Jamii ya
Kitanzania na Taifa la Tanzania la namna gani tuwe navyo 2050;
2050 Mtanzania atakayezaliwa leo na awe ni Kijana aliyeelimika, mwenye afya njema, mwenye Ajira na Kipato, mwenye
kumudu gharama za maisha, na aliye na uhakika wa kesho yake (kwa kuwa na Hifadhi ya
Jamii pamoja na Bima ya Afya).
2050 Jamii ya Kitanzania iwe ni jamii inayoishi kwa Amani, Umoja na Mshikamano, Haki na kujali
Maslahi ya wote.
2050
Tanzania iwe ni Taifa
la Kidemokrasia, lenye
Pato la mtu Mmoja Mmoja (Per Capita) la USD 3,500 na Pato la
Taifa (GDP) la USD 455 Bilioni, Taifa lenye uchumi unaozalisha ajira bora, lenye Amani na Mshikamano.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama wa Zamani, ACT Wazalendo Juni 8, 2024
Dar es salaam
No comments