Breaking News

Serikali yatoa Mil. 250 za dharura kujenga daraja la Mbuga, Ulanga



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu kuipatia TARURA kiasi cha shilingi milioni 250 za dharura kwaajili ya  kujenga daraja la muda la Mbuga katika mto Luhombero pamoja na ukarabati wa daraja la waenda kwa miguu la Chigandugandu wilayani Ulanga yaliyoharibiwa  kutokana na mafuriko.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Mwaya na Mbuga ambao hivi sasa hawana mawasiliano na inawalazimu kutumia mtumbwi wa kuvutwa kwa kamba,Waziri Mchengerwa amesema kwa adha wanayopata wananchi hao daraja la muda haliepukili mahali hapo.

“Ndugu zangu kwanza tupate daraja la muda litakalowawezesha wananchi kupita wao wenyewe pia kupitisha mazao yao katika msimu huu wa mavuno,hatuwezi kutimiza malengo yetu kama daraja hili bovu”.

Waziri Mchengerwa amesema Kwa siku tatu za ziara yake kwenye wilaya zilizopata mafuriko mkoani Morogoro ameshuhudia  maeneo mengi yaliyopata uharibifu mkubwa wa miundombinu na kumuagiza  Katibu Mkuu kuipatia TARURA  milioni 250.

Hata hivyo alitoa maelekezo kwa  TARURA kuanza mara moja mchakato wa dharura wa ujenzi wa daraja hilo na kuwapa mwezi mmoja na nusu kulikamilisha.

Aidha, Waziri Mchengerwa aliwasıhi wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo kwani Rais anaendelea kuwajali wananchi wake na kuiangalia Ulanga hususani kwenye miundombinu.

“Fedha tunazoleta hapa ni fedha za  wananchi ambazo tunaelekezwa na Mhe. Rais,msingi wa serikali ni wananchi”.

Aliongeza kusema kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani itaendelea kuwajali wanyonge pamoja na wananchi wa Mbuga na Mwaya hivyo fedha za dharura zinazotemgwa zinaenda kutibu na  kuimarisha uchumi wa wananchi.

“Rais anawajali wanyonge na wananchi wake ndio maana akatoa fedha hizi kwa ajili kwa wananchi wake hususan maeneo ya uzalishaji na kimkakati ili wananchi waendelee kupata huduma pia wakulima wa mazao ya chakula na biashara waweze kuendelea na shughuli zao”.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameaema daraja hilo ni la kiuchumi pia maisha ya watu wanahitaji daraja hilo kwani wakulima walikuwa wanatumia mtumbwi kuvusha mazao yao.

Amesema ni vyema kuanza kujenga vivuko vya muda katika mkoa wake ili kuweza kuwavusha wananchi na mali zao wakati wanasubiri kujengewa daraja la kudumu.

Awali Mbunge wa Ulanga Mhe. Salim Hasham amesema kata ya Mbuga ina watu wengi na ndio inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la pamba na ufuta ambapo inaifanya Mahenge kuwa na zao la biashara.

Amesema licha ya matatizo ya Ulanga ni makubwa ila tatizo la daraja hilo ni kubwa zaidi  na amemshukuru Waziri kufika eneo hilo ambalo wananchi wa kata ya Mwaya na Mbuga walikuwa wakipata adha ya usafiri hususani wagonjwa.

Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mbuga Mhe. Said Mfaume amesema daraja hilo litakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wananchi wa kata yake kwani kata hiyo inazalisha kwa 75% ya mazao ya biashara na chakula pia wakazi hao hupata huduma za afya upande wa pili wa Kata ya Mwaya.

No comments