MCHANGO WA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA, MHE. LUHAGA JOELSON MPINA (MB) AKICHANGIA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/2025 TAREHE 28 MEI 2024 BUNGENI DODOMA
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Awali ya yote naomba nimpongeze Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Yusuph Makamba (Mb) Naibu Mawaziri, Makatibu Mkuu na watumishi wengine wa Wizara kwa hotuba nzuri yenye taarifa muhimu za kutuwezesha waheshimiwa wabunge kujadili na kufanya maamuzi sahihi juu ya maendeleo ya sekta hii muhimu.
Mheshimiwa Spika, kipekee niwapongeze Waheshimiwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali Duniani kwa kazi nzuri mnayofanya ya kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Diplomasia ya Uchumi. Pia niwapongeze watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kwa namna wanavyochangia maendeleo ya nchi yetu. Hongereni sana.
1. MAMBO YA KIUJUMLA
1.1 Fedha za matumizi ya maendeleo
Katika mwaka wa fedha 2024/2025 fedha zinazoombwa kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Tsh. Bilioni 11.6 sina tatizo na bajeti hiyo. Tatizo langu ni miradi ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi katika miradi ya ujenzi wa ofisi na majengo ya kitega uchumi katika majiji ya Nairobi (Kenya), Lusaka (Zambia) na Kinshasa (DRC) yenye thamani ya Tsh Bilioni 343.1, je ubia huu unatekelezwa kwa vigezo na masharti gani? Na hatua gani imefikiwa hadi sasa? Huu ubia umefikiwaje bila Kamati na Bunge kujulishwa.
1.2 Kukosekana kwa mrejesho wa ajenda zinazosukumwa katika mabunge ya Kikanda na Dunia
Nchi yetu na nchi za Afrika zimekuwa wanachama wa mabunge ya kikanda kama EALA, SADC, PAP, CPA na IPU lakini hakuna mrejesho wa ajenda zinazosukumwa kupitia mabunge hayo, hotuba ya Waziri na ya Kamati hazijasema chochote kuhusu jambo hili. Hivi sasa nchi yetu ina mpaka Rais wa Mabunge ya Dunia (IPU), Mhe. Dk.Tulia Ackson (Mb).
Pia nchi yetu iliwahi kuwa na Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Mhe. Getrude Mongela (Mb), Makamu wa Rais wa PAP, Mhe Stephen Masele (Mb), Katibu Mtendaji wa Mabunge ya CPA, Mhe. Dk. William Shija (Mb), Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Dk. Stergomena Tax (Mb) na wengine wengi.
Nchi wanachama zinatumia fedha nyingi za walipa kodi kugharamia vikao katika mabunge hayo na hivyo isingetarajiwa mijadala inayoendelea katika mabunge hayo kuwa ya siri na Waziri wa Mambo ya Nje ameishia kuripoti utendaji kazi wa Bunge moja tu la EALA.
1.3 Kutokulipwa fidia kwa Askari wanaoshiriki
Operesheni za kulinda amani nje ya nchi
Askari wetu wa Tanzania wanapochukuliwa katika misheni mbalimbali za operesheni za kulinda amani kama SADC, EAC,
MUNUSCO nk, familia za walinda amani kutoka nchi wanachama waliopoteza maisha au kupata ulemavu katika operesheni za ulinzi wa amani na mazoezi ya kijeshi nje ya nchi wamekuwa hawalipwi fidia na kuziacha familia zao kwenye ufukara wa kutupwa. Nchi yetu hadi Machi 2024 ina walinda amani 1,537 ikishika nafasi ya 11 katika ya nchi 119 zinazochangia walinda amani katika misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. 1.4 Madereva wanaosafirisha mizigo nje ya nchi
Madereva hawa husafiri masafa ya mbali huku wakiwa wameacha familia zao na kuwa kwenye hatari kubwa za kiusalama na pengine sheria hutofautiana nchi na nchi kama kuzuia baadhi ya bidhaa kuingia nchi nyingine, uzito wa mzigo na sheria zingine za barabarani lakini pia kutekwa na ajali.
Lakini pamoja na hayo yote madereva wetu na vijana wetu wanaendelea kulitetea taifa lao kwa kuhakikisha kuwa mizigo yote inafika panapohusika kwa majirani zetu nchi za Rwanda, Burundi, DRC Congo, Zambia, Kenya, Malawi, Zimbabwe, Uganda nk.
Madereva hawa kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kutokuwa na Mikataba ya ajira baina yao na matajiri, kutokuwa na Bima, kulipwa masurufu kidogo yanayopelekea kushindwa kujikimu wawapo safarini na kuhudumia familia zao. Familia kuachwa kwenye dhiki kubwa inapotokea vifo na ulemavu unaosababishwa na ajali au kutekwa. Waziri wa Mambo ya Nje atueleze ni mkakati gani uliopo wa kuhakikisha madereva hawa wanapata maslahi mazuri na kuwakinga dhidi ya majanga ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
1.5 Kukosekana kwa mtandao mpana wa utoaji habari (Massive Coverage)
Nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla hazina mkakati wa pamoja wa kutangaza mambo ya ndani ya nchi husika na kubadilishana taarifa kama ilivyokuwa miaka ya mwanzoni mwa Uhuru ambapo kila nchi iliripoti mambo ya nchi zingine za Afrika.
Licha ya mageuzi makubwa ya Teknolojia ya Habari kiwango cha kubadilishana habari ni kidogo sana na hivyo kila nchi imejifungia na mambo yake. Nakumbuka waasisi wetu walitumia vyema Redio na Magazeti kudai Uhuru, mfano Redio ya Taifa ya Kenya (KBC Nairobi) ilisikika maeneo mbalimbali ya Tanzania hadi vijijini lakini leo maeneo mengi Redio hiyo haipatikani.
Nawakumbuka Watangazaji maarufu wa KBC Nairobi kama Leonard Mambo Mbotela katika kipindi chake maarufu cha Je huu ni Uungwana? mambo yalikuwa mazuri sana. Na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) nayo ilisikika maeneo mbalimbali ya nchi jirani. Licha ya mageuzi makubwa ya TEHAMA mambo yamegeuka mtandao wa mawasiliano Afrika Mashariki na Afrika umekatika vimebaki vyombo vya habari vya kimataifa ambavyo navyo huripoti mambo mabaya tu kama mizozo na machafuko, vita, njaa, mafuriko, ukame katika nchi za Afrika.
Ilitegemewa suala hili la kuziunganisha nchi za Afrika katika mawasiliano ingekuwa ni ajenda muhimu kwa mawaziri wa mambo ya nje na Serikali za Umoja wa Afrika. Lakini hatujaona mkazo wowote kwenye eneo hili. Kwa nchi yetu yenye mtandao mrefu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hii ni fursa muhimu, ingawa pia kwa siku za hivi karibuni hadi Bunge linakatiwa matangazo ya moja kwa moja (live coverage) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na chombo hicho kujiunga na kuripoti matukio ya warsha, makongamano na ziara za Viongozi. Kwa Mamlaka lililopewa Bunge katika Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Rais akiwa ni sehemu yake usingetegemea Shirika la Umma la TBC kudharau shughuli za Bunge.
Aidha kipekee niipongeze sana Kampuni ya Azam Media ambayo mtandao wake unazidi kusambaa kila siku na kuzihudumia nchi jirani za Kenya, Uganda, Zimbabwe na Malawi. Lakini pia jambo kustaajabisha AZAM Tv ambacho ni chombo binafsi lakini kinalipa heshima na uzito unaostahili Bunge la Tanzania kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja (live coverage) bila kukatakata kuanzia kipindi cha maswali na majibu saa 3 asubuhi hadi saa 7 kamili mchana. Nawapongeza sana Azam Tv mnalipa heshima Bunge letu na Taifa letu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
2. UMOJA WA AFRIKA
Ushirikiano wa Nchi za Afrika ulianza mapema katika kipindi cha mapambano ya ukombozi wa mataifa ya Afrika kutoka kwenye makucha ya Wakoloni ambapo nchi za Afrika ziliungana kwa pamoja kudai Uhuru kutoka kwa Waingereza, Wajerumani, Wafaransa, Makaburu, Waarabu nk.
Hatujasahau namna waasisi wetu walivyojitoa kwa hali na mali kupigania Uhuru wa Bara la Afrika hadi nchi zote za Afrika zikapata Uhuru. Viongozi wetu mashuhuri (Illustrious Leader) wakiongozwa na Kwame Nkrumah, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Jomo Kenyata, Samora Machel, Nelson Mandela, Sam Nujoma, Kenneth Kaunda, Robert Mugabe, Thomas Sankara na wengine wengi.
Viongozi hawa walifanya kazi kubwa ya kuzipatia Uhuru nchi zetu, kuweka mifumo ya utawala, Kukuza uchumi ambapo njia kuu za uchumi zilirejeshwa na kumilikiwa na umma na vita dhidi ya maadui Ujinga, Umaskini na Maradhi vikatangazwa. Tumekuwa tukiendelea kushuhudia ustawi wa nchi za Afrika tangu mapambano yalipoanza.
Katika kuendeleza mapambano hayo nchi za Afrika zimeungana katika kanda mbalimbali ikiwemo AU, EAC, COMESA, SADC nk. na ajenda mbalimbali zimekuwa zikiwekwa na kutekelezwa. Mfano Dira ya Maendeleo ya Afrika (Agenda 2023- The Africa we Want), APRM na Misheni mbalimbali.
Pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto nyingi zinazokwamisha ustawi wa Bara ya Afrika.
Matatizo sugu barani Afrika
Pamoja na mafanikio tuliyoyapata Afrika Mashariki na Afrika lakini zipo baadhi ya changamoto ambazo binafsi naona bado hazijashughulikiwa kikamilifu na hivyo kuhitaji mikakati mipya, maarifa mapya na mbinu mpya katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo. Naomba kutoa mifano tisa (9) kama ifuatavyo:-
2.1 Mapigano na uvamizi wa magaidi baina ya nchi za
Afrika Mashariki na Afrika
Baadhi ya nchi zimekuwa zikikabiliwa na migogoro inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na tofauti za kiitikadi, kudorora kwa uchumi, ugaidi, mizozo na machafuko ya kisiasa. Hali ambayo imekuwa ikipelekea vifo, majeruhi, njaa, wakimbizi na wahamiaji haramu, ongezeko la uhalifu unaovuka mipaka, mateso ya kina mama na watoto, nk
Tumekuwa tukishuhudia mapigano yasiyokwisha Mashariki mwa Congo baina ya majeshi ya Serikali ya Congo (FARDC) na vikundi vya waasi ikiwemo Vikosi vya M23 ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Hatua zinazochukuliwa, tumekuwa tukishuhudia tume za upatanishi na misheni za ulinzi wa amani za kijeshi zimekuwa zikiundwa kutoka, EAC, SADC, SAMIM, AU, FIB na Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) ili kukomesha mapigano hayo na kurejesha amani Mashariki mwa Congo. Lakini jambo la kusikitisha mapigano hayo yanazidi kupamba moto kila uchao.
Pia huko Kaskazini mwa Ethiopia mapigano yamekuwa yakiendelea baina ya majeshi ya Serikali na waasi (Tigray rebels) katika vita maarufu ya Tigray War. Huko Somalia chokochoko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe (Somalia Civil War) na uvamizi wa magaidi hali inayoleta machafuko ya mara kwa mara katika nchi hizo na kuhatarisha usalama wa raia wake na nchi jirani. Tumeshudia pia kuwepo kwa Machafuko huko Msumbiji, Libya, Mali, Morocco, Saharawi, Sudan nk. Ni ukweli usiopingika kuwa kukosekana kwa amani katika nchi hizo ni kukosekana kwa amani kwa Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla.
Maswali ya kujiuliza kwanini mapigano hayakomi na kwanini amani hairejei katika maeneo hayo licha ya hatua zinazochukuliwa na UN, AU, SADC na EAC? Binafsi naona nchi za Afrika Mashariki na mamlaka zingine hazijawekeza kikamilifu kushughulikia mizizi ya machafuko hayo ili kukomesha mapigano na kurejesha amani.
Tulishuhudia Kiongozi wa Kundi la Kigaidi la Al Qaeda, Osama Bin Laden alipofanya shambulio la kigaidi katika jengo refu la World Trade Centre mjini New York nchini Marekani tarehe 11 Septemba 2001 na kusababisha vifo vya watu 3,000, nchi ya Marekani chini ya Rais George W. Bush na marafiki zake ikiwemo Uingereza chini ya Waziri Mkuu wa wakati huo Tony Blair ambapo walitangaza vita dhidi ya magaidi kote duniani na wakaapa kuwa hawatapumzika hadi ugaidi utokomezwe na kurejesha amani duniani kote.
Baada ya hapo tukaanza kushuhudia mapigano makali ya vita dhidi ya ugaidi pamoja na mtandao wake wa Al Qaeda, mashambulio makali yalifanywa na majeshi ya Marekani, Uingereza na NATO katika nchi za Pakistan na Afghanistan ambako ndiko ilikuwa hifadhi ya magaidi. Hatimaye tulisikia kuwa Osama Bin Laden ameuawa na mtandao wake wa Al Qaeda wote kuteketezwa na amani Duniani kurejea.
Viongozi hawa walijua athari za kuenea ugaidi duniani na ndiyo maana walitangaza na kupigana vita na walikataa suluhu ya aina yoyote. Leo kwanini machafuko ya rejareja yaruhusiwe katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla? Mizozo, machafuko na mapigano yanayoendelea yanarudisha nyuma jitihada za nchi za Afrika kujiletea maendeleo.
Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika mko wapi haya yanaendelea? Dk. Samia Suluhu Hassan Mwanamke Shupavu, Dk. William Ruto Msomi Kiongozi Bara la Afrika, Yoweri Kaguta Museveni, Rais Mkongwe mko wapi haya yanaendelea.
Umoja wa Afrika umezisimamisha nchi 6 kushiriki shughuli za Umoja wa Afrika kutokana na mapinduzi ya Serikali katika nchi hizo ambazo ni Burkina Faso, Gabon, Guinea, Mali, Niger na Sudan, ushauri wangu kwa AU nchi hizi hazikupaswa kusimamishwa kushiriki vikao kwani kwa sehemu kubwa watawala waliopinduliwa kwenye nchi hizo walijitakia wenyewe kwa kushindwa kusimamia utawala bora, mgawanyo usio sawa wa raslimali, ukosefu wa ajira, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ongezeko la umasikini. Badala yake AU isisitize Serikali za nchi wanachama kuzingatia utawala wa Sheria na Utawala bora ili zisiendelee kupinduliwa.
2.2 Ufisadi, Rushwa na matumizi mabaya ya raslimali
Kutokana na kushamiri kwa rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za asili nchi nyingi za Afrika umasikini unazidi kuongeza licha ya utajiri mkubwa tulionao wa raslimali kama bahari, maziwa, mito, madini, ardhi yenye rutuba, mifugo, wanyama, misitu, gesi asilia, mafuta nk. nchi nyingi zinakosa mapato ya kutosha kwa ajili ya maendeleo na kuendesha nchi kwa sababu fedha na raslimali za umma ziko mikononi mwa watu binafsi huku nchi kwa sehemu kubwa zinategemea misaada na Mikopo kutoka nje.
Kukosekana kwa mifumo madhubuti ya Usimamizi na udhibiti wa mapato, matumizi na raslimali za umma hali inayopelekea fedha za umma kuishia mikononi mwa watu wachache. Chanzo kikubwa ni uingiaji wa Mikataba Mibovu, Utoroshaji wa rasilimali na fedha nje ya nchi (Illicit Financial Flows), Transfer Pricing, Capital Flight, wizi, rushwa na ufisadi ni kidondandugu kilichokosa tiba barani Afrika.
Pamoja na kuwepo Sheria, wakaguzi wa ndani na nje, Mamlaka za Kudhibiti na Kupambana na Rushwa, kuanzishwa kwa vitengo vya FIU na EITI, APRM na mamlaka zingine za Usimamizi wa Sheria lakini hali bado ni mbaya ya wizi, rushwa na ufisadi Afrika.
Baadhi ya nchi za Afrika zinakusanya kodi kwa uwiano wa pato la taifa chini ya kiwango kinachokubalika cha 15%, mfano Tanzania inakusanya 12.5% tu, Uganda 13.3%, Kenya 14.2% ya Pato la Taifa. Na hivyo kukosekana mapato ya kutosha kugharamia shughuli za maendeleo na uendeshaji wa Serikali. Nchi zote za Afrika Mashariki zina nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada kinachozidi 3% ya pato la taifa. Nchi nyingi za Afrika zina mfumko wa bei unaozidi 8% na akiba ya fedha za kigeni isiyotosheleza mahitaji ya miezi 4.
Mfano Tanzania inaripotiwa kutorosha nje ya nchi zaidi ya Tsh Trilioni 3.5 kwa mwaka na Kenya inaripotiwa kutorosha zaidi ya Ksh 40 bilioni (sawa na Tsh Bilioni 744) kwa mwaka. Swali la kujiuliza ni kwanini mianya ya upotevu wa mapato na raslimali za nchi imeshindwa kudhibitiwa barani Afrika?
2.3 Mikopo na Misaada
Nchi nyingi za Afrika zimetumbukia kwenye mzigo mkubwa wa madeni (Highly Indebted Poor Countries-HIPC) na mikopo hiyo inatolewa kwa masharti magumu na ya kinyonyaji. Nchi nyingine kuchukua mikopo inayolindwa na dhamana ya maliasili za nchi kama madini, gesi, mafuta, bandari nk, kuingiliwa katika utungaji na Usimamizi wa sera, sheria, kanuni, miongozo, program na mikakati na hivyo kunyang’anywa uhuru wa kujiamulia mambo wakati mwingine kutekeleza miradi ambayo haipo kwenye vipaumbele vya nchi ili kukidhi matakwa ya wahisani, mikopo kukosa uwazi, ulinganifu na yenye riba kubwa na masharti mengi ya kinyonyaji na kusababisha mfumko mkubwa wa bei za bidhaa.
Mikopo ya aina hii imezifanya nchi nyingi za Afrika kufilisika na kurudi nyuma kiuchumi na kuendelea kuishi kwa kutegemea misaada na mikopo na kupelekea kuongezeka kwa migogoro ya kifedha hasa inapotokea ugumu wa kurejesha mikopo hiyo. Kwanini nchi za Afrika zimeshindwa kujenga uchumi imara na kuendelea kutegemea misaada na mikopo. Bw. Donald Kaberuka, Gwiji wa uchumi huko nchini Rwanda aliwahi kusema waafrika tunatakiwa kugundua namna ya kutumia raslimali zilizopo katika bara ya Afrika ili kuibadilisha Afrika.
Nchi nyingi hukusanya kodi chini ya 15% ya pato la Taifa na kuendelea kutegemea mikopo na misaada ambapo kumepelekea nchi nyingi za Bara la Afrika kuwa na madeni makubwa ya nje kiasi cha kushindwa kuendelea kukopesheka na kusababisha matatizo makubwa kwenye nchi hizo. Nchi nyingi zimefikia kiwango cha juu cha Deni la Taifa kinachozidi 50% ya pato la taifa. Hii inasikitisha sana kwa nchi za Afrika mapato yake kumezwa na mirija ya wizi, rushwa na ufisadi na kuendelea kutegemea mikopo na misaada kutoka nchi zingine.
Wakuu wa nchi na Serikali za Umoja wa Afrika wana mipango gani ya kufanya mageuzi katika kuweka mikakati mipya ya kuondokana na mtego huu wa madeni katika nchi za Afrika.
2.4 Uwekezaji na biashara katika nchi za Afrika Mashariki
Shughuli za uwekezaji na biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mafanikio tuliyoyapata bado zina changamoto nyingi licha ya uwepo wa Itifaki ya Umoja wa Forodha (EAC- Common External Tariff), Itifaki ya Soko la Pamoja na Itifaki ya Sekta za Uzalishaji na Miundombinu zilizowekwa kwa ajili ya kuongeza kasi ya kufufua uchumi na kuimarisha sekta za uzalishaji katika jumuiya. Pia mikakati mingi imekuwa ikiwekwa kama kuanzishwa kwa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) na eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kwa lengo la kuongeza kasi ya biashara na uwekezaji, kuongeza uzingatiaji wa viwango na ubora wa bidhaa, kuongeza thamani na kupanua soko la bidhaa. Lakini bado nchi za Afrika zinaendelea kuwa soko la bidhaa kutoka nje na zenyewe kukazana kuuza malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.
Hotuba ya Waziri katika Ibara ya 100 inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania katika mwaka 2023/2024 ilisaini Jumla ya Mikataba na hati za Makubaliano 78 baina ya Tanzania na nchi za mbalimbali za Afrika na nchi zingine duniani bila kueleza kwa kina Mikataba na Makubaliano hayo ni kwa ajili ya nini, nchi yetu inaenda kunufaika namna gani katika mikataba hiyo.
Mfano hutuba ya Waziri inasema imeingia Mikataba 11 ya Nishati, 2 ya madini, 11 ya elimu, ni katika maeneo gani hasa? Lakini tunajua Mikataba mingine inahusu raslimali za taifa ilipaswa kuletwa Bungeni.
2.4.1 Mashirikiano ya Kibiashara baina ya nchi za Afrika Mashariki na Afrika
Mashirikiano ya Kibiashara baina ya nchi za Afrika Mashariki (Intra -EAC Trade) ni mazuri japo yana changamoto nyingi hususan biashara za Serikali na Serikali ambapo baadhi ya nchi zinaagiza bidhaa kutoka nje ya ukanda wa EAC, SADC, COMESA, AU nk. hata kwa bidhaa ambazo zinapatikana ndani ya kanda husika. Mfano Mchele, ngano, mahindi, samaki, nyama, maziwa, matunda na mbogamboga, mafuta ya kupikia, sukari, mashudu, wanyama hai na mazao ya misitu kama samani, karatasi, pia vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, vigae, chuma na plastic, mifumo ya TEHAMA nk. Mfano Tanzania inauza nchini Kenya wastani wa 3.8% tu ya thamani ya mauzo kwa mwaka.
Kuchelewa kwa matumizi ya Sarafu moja katika nchi za Afrika Mashariki, vikwazo visivyo vya kikodi na ukosefu wa mitaji unachangia kwa kiwango kikubwa kuzorota kwa uwekezaji na biashara. Ubinafsi huu unazifanya nchi za Afrika Mashariki na Afrika kutokufanya vizuri zaidi katika biashara za kikanda. Mimi naamini kwamba kukosekana kwa mashirikiano thabiti ya Kibiashara inatokana na kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
Tumekuwa tukifanya vibaya katika eneo hili licha ya kuwepo kwa Itifaki ya Soko la Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayosisitiza kuongeza uzalishaji na kiwango cha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya.
2.4.2 Kuuza malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani
Nchi nyingi za Afrika Mashariki zinauza malighafi katika Masoko ya Afrika Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), India, China, Uswisi na Masoko ya AGOA na kuuza kiasi kidogo sana katika Masoko ya EAC, SADC, COMESA, ECOWAS nk.
Hali hii inazifanya nchi za Afrika Mashariki kutonufaika kikamilifu na rasilimali zake. Ni kitu cha kusikitisha sana kwamba tunasafirisha nje ya nchi mbegu za mafuta halafu tunaagiza mafuta ya kupikia kwa gharama kubwa, tunasafirisha nje ya nchi pamba ghafi halafu tunaagiza nguo kwa gharama kubwa, tunasafirisha magogo alafu tunaagiza karatasi, samani, nguzo za umeme kwa gharama kubwa, Tunaagiza mbolea matani kwa matani wakati tuna samadi na mboji zikioza ardhini nk. Ipo mifano mingi inaumiza sana.
Mimi naamini kwamba hakuna kizuizi kinachofanya nchi za Afrika zisijenge viwanda vya kuongeza thamani mazao, hivyo kitendo cha kuendelea kuuza malighafi katika masoko ya Ulaya, Asia, Marekani na Masoko mengine ni kukosekana kwa dhamira ya dhati. Pamoja na kuwepo kwa utekelezaji wa program za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika sekta za uzalishaji, miundombinu ya uchumi lakini bado tunafanya vibaya katika eneo hilo.
2.5 Kuchelewa na kusuasua kwa utekelezaji wa
maazimio, Itifaki na Makubaliano
Kumekuwepo na Itifaki, maazimio na Makubaliano mbalimbali ambayo yamekuwa yameridhiwa katika vikao halali vya AU, SADC, EAC nk. lakini uridhiwaji na utekelezaji umekuwa wa kusuasua na kurudisha nyuma kasi ya maendeleo katika nchi za Afrika.
Pamoja na tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa kwanza wa miaka 10 ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Afrika (Agenda 2063, The Africa we Want) lakini matokeo ya tathmini hiyo kuhusu mafanikio, fursa na changamoto hayawekwi wazi na wakuu wa nchi na Serikali na Umoja wa Afrika ili kutoa fursa ya kujipima hatua iliyofikiwa.
2.6 Tatizo la ajira
Nchi za Afrika kupitia Umoja wa Afrika zimeweka mikakati, program na kuchukua hatua mbalimbali ili kutatua tatizo la ajira katika bara la Afrika (Youth Employment Intervention in Africa) Lakini badala yake tatizo la ajira linazidi kuongezeka kila siku. Nchi za Afrika zimeanzisha Umoja wa Vijana (Pan African Youth Union-PYU) na pia kuingia katika makubaliano (The African Youth Charter) ili kuweka mikakati na misingi ya kisheria itakayowezesha kusukuma ajenda ya upatikanaji wa ajira ya vijana katika bara la Afrika.
Serikali za nchi wanachama, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi nazo hazijarudi nyuma katika mapambano ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Pia nchi wanachama zinapata msaada mkubwa kutoka ILO na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kutengeza ajira za vijana. Hata hivyo nchi za Afrika bado hazijafanikiwa kutatua tatizo la ajira kwa vijana, Ukipitia utekelezaji wa MDGs na SDGs. Unathibitisha wazi kuwa nchi za Afrika zinahitaji mikakati mipya kupambana na hali ya ukosefu wa ajira kwa vijana katika sekta za umma na sekta binafsi.
Baadhi ya sababu zinazosababisha hali kuendelea kuwa mbaya zaidi ni kama ifuatavyo:-
(i) Kukosekana Sera na Sheria madhubuti za kulinda na kutengeneza ajira za wazawa katika Bara la Afrika,
Sheria na Sera zilizopo zinakinzana na hazitoi ulinzi wa kutosha kulinda ajira. Mfano Manunuzi, local content na Mikataba inayoingiwa. Katika Sekta ya Ujenzi miradi mingi imechukuliwa na wageni yaani kila mradi ni wao mfano Kampuni ya CCECC na CRJE kutoka China kila mradi wapo iwe miradi ya maji, barabara, Ujenzi wa SGR, Madaraja, Bandari nk.
(ii) Kukoseka kwa mifumo ya udhibiti hali inayopelekea kushamiri kwa biashara za magendo, kugeuzwa kuwa dampo za bidhaa hafifu na zilizokwisha muda wa matumizi, kukwepa kodi na hivyo kupelekea kuua viwanda vya ndani na ajira.
(iii) Sekta kubwa zinazoajiri waafrika wengi kutopewa kipaumbele katika mipango na bajeti za nchi wanachama kama Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Madini, kukosekana kwa viwanda vya chakula, nguo, dawa, ngozi, viatu, nyama, maziwa, mbolea. Huku wanaochimba madini kwa sehemu kubwa sio waafrika na hao wachache wachimbaji wadogo wanakutana na hujuma za kila aina. Hii inapelekea nchi nyingi za Afrika kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje huku ikiuza bidhaa zake kama malighafi kwa mataifa ya nje tena kwa bei ya kutupa na kuua ajira nchini.
(iv) Mifumo dhaifu ya elimu na ujuzi, mitaala na namna tunavyowandaa vijana wanashindwa kukidhi mahitaji ya soko la ajira, wanakosa ujuzi na maarifa ya kuajiriwa na kujiajiri. Hata mageuzi makubwa ya TEHAMA yameshindwa kuwa suluhisho la upatikanaji wa ajira katika bara la Afrika.
2.7 Umasikini na maradhi
Licha ya mikakati inayowekwa kitaifa na kimataifa kama malengo ya MDGs, SDGs nchi nyingi za Afrika zilishindwa kufikia malengo hayo, nchi zingine umasikini umepungua kwa kiwango kidogo na zingine umasikini unazidi kuongeza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Usimamizi hafifu wa Sera za Fedha na Bajeti, mizozo na machafuko ya kisiasa, ukosefu wa ajira, wizi, rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za nchi.
Lakini pia kumekuwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama Figo, Moyo, Kisukari, Saratani, Shinikizo la Damu nk. magonjwa haya yanaongezeka kwa kasi kila uchao lakini hakuna tafiti za kitabibu (Medical Reaserch) zilizofanywa ili kujua kiini cha tatizo na hatua za kudhibiti magonjwa hayo.
HITIMISHO
Tunataka Afrika yenye amani na utulivu, tunataka Afrika yenye mageuzi makubwa ya maendeleo na uchumi na ustawi wa watu wake, hivyo ni lazima kufanyia kazi usiku na mchana kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo sugu yanayolikabili bara la Afrika. Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika waandae mikakati mipya na kuitekeleza kwa ujuzi na maarifa mapya na tukaionyeshe dunia uelekeo mpya.
Ninatambua kazi nzuri inayofanywa na nchi wanachama na Umoja wa Afrika (AU) katika kufikia maendeleo ya kweli ambapo pia Tume na misheni mbalimbali zimekuwa zikiundwa. nimuombe Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU) na Rais wa Mauritania Mhe. Mohamed Ould Cheikh Gazouani aridhie kuunda Tume ya kuandaa mikakati mipya ya namna ya kukabiliana na matatizo sugu barani Afrika na ikimpendeza aniteue mimi Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Jimbo la Kisesa niwe miongoni mwa wajumbe wa tume hiyo ili nami nitoe mchango wangu kwa Bara langu la Afrika na dunia.
Nawasilisha,
Luhaga Joelson Mpina (Mb) Mbunge wa Jimbo la Kises
No comments