MATUMIZI HUDUMA ZA MAWASILIANO YAONGEZEKA,LAINI ZA SIMU MILIONI 72.5 ZIMESAJILIWA HADI MACHI 2024
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema hali ya
mawasiliano katika robo inayoishia machi 2024 imeonesha maendeleo makubwa kwa
kuongezeka kwa utumiaji wa huduma za mawasiliano, ikichochewa na ushindani
endelevu wa bei za huduma.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA
Dkt. Jabiri Bakari akizungumza katika kikao cha mashauriano kati ya TCRA na
Wahariri wa Vyombo vya Habari vya Magazeti kuhusu takwimu za huduma za Mawasiliano
ya Simu yaliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Mathalani Dkt. Bakari akifafanua kuhusu takwimu za
usajili wa laini za simu, alisema laini
zilizosajiliwa imeongezeka kutoka milioni 70.3 katika robo ya mwaka iliyoishia
Disemba 2023 hadi milioni 72.5 kwa robo inayoishia Machi 2024 hilo likiwa ni
ongezeko la asilimia 3.1.
Alibainisha kuwa laini hizo ni za simu za mkononi na
simu za mezani ambazo zimetumika angalau mara katika miezi mitatu iliyopita.
“Moja ya mafanikio hayo ni kuenea kwa mtandao wa simu
za mkononi katika teknolojia mbalimbali, ambapo mtandao wa 3G umeenea kwa 88%
ya watu, na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya Intaneti,” alisema Dkt.
Bakari.
Kwamba kuenea kwa mtandao wa 4G kwa asilimia 80 ya
watu kumeongeza kasi na upatikanaji wa uhakika wa huduma ya Intaneti, wakati uo
huo, 5G imeenea kwa asilimia 13 ya watu huku ikileta zama mpya ya mtandao wa
kasi ya juu ambayo ni muhimu kwa mahitaji ya Intaneti ya kasi.
Dkt. Bakari alisema mafanikio hayo yameambatana na uboreshaji
wa huduma za mawasiliano, udhibiti wa majaribio ya ulaghai na uimarishaji wa
miundombinu ili kufikia Uchumi wa kidijiti.
Kadhalika, alibainisha kuwa Sekta ya utangazaji
ilipata mwelekeo mzuri wa ongezeko la asilimia 2.5 la visimbuzi ikilinganishwa na
robo mwaka iliyopita ambapo ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa ubora wa
huduma kwa wateja wa huduma ya utangazaji.
Alisema maboresho hayo ya pamoja katika sekta ya
mawasiliano ni muhimu katika kukuza jamii iliyounganishwa na iliyowezeshwa
kidijitali.
No comments