Breaking News

Tuulinde Muungano Wetu kwa Gharama Yoyote: Mhe. Abdulla Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla

Na Georgina Misama, Maelezo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Watanzania kuulinda na kuuheshimu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa gharana yoyote na kwamba si jambo rahisi kudumu kwa miaka 60 ya kuwa pamoja kwa amani na utulivu.

Mhe. Abdulla amesema hayo  leo Aprili 19, 2024 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wakati akizindua Maonesho ya Taasisi za Muungano kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungazo wa Tanzania ambapo alisema, taasisi za muungano zimekuwa na ufanisi katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano.

“Tukumbuke kuwa, muungano wetu umedumu kwa miaka 60 sasa na hatuna budi kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha, tupime tulikotoka na tuangalie tunakoelekea miaka ijayo, tunayo haja ya kuendelea kusoma na kujifunza juu ya muungano wetu,” alisema Mhe. Abdulla.

Aidha, aliongeza kuwa, taasisi za muungano zimefungua Ofisi Tanzania Bara na Zanzibar ambao hadi sasa, taasisi 33 zimefungua ofisi Zanzibar kati ya taasisi 39 za muungano na kwamba hiyo ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma kwa wananchi na kuimarisha muungano, aidha alitumia fursa hiyo kuzipongeza taasisi za muungano zilizo na ofisi Zanzibar na kutoa wito kwa zile ambazo bado hazijafungua ofisi kufanya hivyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Hamis Hamza Hamis alisema uchumi umeimarika kutokana na mazingira na mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, aidha, kuimarika kwa miundombinu, hususan ya barabara na huduma za jamii ikiwamo afya, maji na elimu katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili za muungano.

“Watanzania tunafurahia muungano huu umetuletea mafanikio mbalimbali katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa wananchi pande zote mbili za muungano.  Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na uhuru wa kuishi kwa amani na utulivu sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii bila bughudha yoyote,” alisema Mhe. Hamza.



No comments