Breaking News

Tanzania na Urusi kushirikiana kudhibiti Uhalifu wa Kimtandao

 

Na Mwandishi Wetu, URUSI

Serikali imedhamiria kushirikiana na nchi ya Urusi katika kudhibiti uhalifu nchini ikiwemo uhalifu wa  mtandao ambao umeanza kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini huku ikiweka wazi dhamira ya kujengewa uwezo kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na nchi zilizoendelea kiteknolojia katika kudhibiti uhalifu huo unaotajwa kuvuka mipaka.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi HamadMasauni wakati wa   Mkutano wa Kimataifa wa Maafisa wa Daraja la Juu kutoka serikalini wanaohusika na mambo ya Usalama unaoendelea nchini Urusi ambao ulifunguliwa na Rais wa Shirikisho la Urusi na kuongozwa na Katibu wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Urusi, Nikolai Patrushev.


‘Katika kudhibiti masuala ya uhalifu wa kimtandao matumizi ya teknolojia hayaepukiki ndio maana serikali imeona kuna haja ya kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ujuzi kwa askari wetu sasa kupitia mkutano huu tunaenda kujenga mahusiano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Urusi ili tuweze kudhibiti uhalifu wa kimtandao ambao umekua ukisababisha madhara mbalimbali katika jamii ikiwemo ya kiusalama,kiuchumi na hata maadili’. Alisema Waziri Masauni

Akizungumza wakati wa Mkutano huo Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Miriam Mmbaga alisema muelekeo wa wizara katika kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ina mkakati maalumu wa kuwajengea uwezo askari waliopo katika Vyombo vya Ulinzi hasa katika masuala ya teknolojia huku akiweka wazi juu ya suala la ajira pia kuweka kipaumbele kwa watu waliosomea masuala ya teknolojia ya Habari.

Mkutano huo wa Kimataifa wa Maafisa wa Daraja la Juu kutoka serikalini wanaohusika na mambo ya Usalama umehudhuriwa na nchi takribani 20 huku msisitizo zaidi ukiwekwa katika kupambana na uhalifu wa kutumia teknolojia ambao umekua ni tishio katika mataifa mbalimbali.


No comments