Serikali kupitia TBS hutenga zaidi ya milioni 250 kuhudumia wajasiriamali
Yatoa leseni za ubora wa bidhaa 2,106 kwa kipindi cha
miaka mitatu
NA Tunu Bashemela
SERIKALI kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
imekuwa ikitenga zaidi ya shilingi milioni 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali
wadogo bila ya malipo yoyote.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt.
Athumany Ngenya akizungumza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu
utekelezaji, majukumu na mafanikio ya Shirika hilo.
Kuhusu utoaji wa leseni za Alama ya Ubora, Dkt. Ngenya
alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106
zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3
ya lengo la kutoa leseni 2,000.
“Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa
bure na kwa Wajasiriamali wadogo. Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya
viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa
sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango hivyo
viliandaliwa katika Nyanja mbalimbali,” alisema Dkt. Ngenya.
Kwamba TBS imeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara
vya Afrika Mashariki na Afrika nzima.
Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabatho Kosuri, akizungumza alipokuwa akitoa neno la utangulizi katika mkutano huo.
Akizungumzia kuhusu mafunzo kwa Wazalishaji na Wajasiriamali
Dkt. Ngenya alibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya wadau 5,789
kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo hayo.
Kwamba TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali
wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi
matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko
ya ndani, kikanda na kimataifa.
Dkt. Ngenya alisema katika ukaguzi wa bidhaa
zinazozalishwa nchini, Shirika limeandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote
hapa nchini ili kuhakikisha kwamba vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.
Hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za
ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa
nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.
Alisema, TBS katika utekelezaji wa majukumu yake
imepata mafanikio kadhaa ikiwemo ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga
Maabara katika Mikoa ya kimkakati
Kwamba Shirika linatekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu
ya Shirika na maabara (Viwango House-Dodoma) ambapo Maabara hii itahudumia
mikoa mitatu (3) ya kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na
mikoa mingine ya karibu.
Dkt. Ngenya alibainisha kuwa, Shirika linatarajia
kuanza ujenzi wa maabara yakisasa katika kanda ya Ziwa (Mwanza) na kanda ya
kaskazini (Arusha) huku Maabara ya kanda ya ziwa ikitarajiwa kuhudumia mikoa
sita (6) ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Aliendelea kueleza, Maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa
kuhudumia mikoa minne (4) ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Mafanikio mengine ni kuongeza na kuimarisha ofisi za
kanda, kwamba Shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia
ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha) ,Kanda ya Kusini (Mtwara)
,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya
ziwa (Mwanza), Kanda ya Kati (Dodoma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).
Kwamba Kanda hizi zina ofisi katika mipaka, bandari pamoja
na viwanja vya ndege.
Kadhalika alisema TBS imefanikiwa kuongeza ufanisi
katika utoaji huduma ikiwemo ununuzi wa mashine za kisasa za maabara.
Alifafanua kuwa, Shirika limewekeza kwenye ununuzi wa
vifaa vya maabara vya kisasa (state-of-the-art-equipment) kwa kutumia fedha za
ndani pamoja na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kuhusu, ithibati za umahiri katika maabara, alisema Shirika
lina maabara 12 zilizopo Ubungo Dar es Salaam, maabara hizo zimehakikiwa na
kupatiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa kimataifa (accreditation).
Alisema hatua hiyo inapelekea majibu ya sampuli kutoka
katika maabara hizo kuaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara.
Wahariri na Waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya akieleza mafanikio ya taasisi yake katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano uliofanyika leo Aprili 15,2024, Jijini Dar es Salaam, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
No comments