Breaking News

MBUNGE MTATURU ALIA NA UJENZI MADARAJA SINGIDA MASHARIKI


SERIKALI inatambua umuhimu wa vivuko na madaraja katika Jimbo la Singida Mashariki ambapo kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imeweka katika mpango wake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya Shilingi Bilioni 1.11 kwa ajili ujenzi wa madaraja katika Wilaya ya Ikungi.

Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Zainab Katimba amesema hayo Aprili 8,2024,Bungeni Jijini Dodoma,wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.

Katika swali lake Mtaturu ametaka kujua ni lini serikali itajenga Maradaja kwenye Barabara za Misughaa-Kikio na Matongo - Mpetu - Singida.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Katimba amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024,jumla ya Shilingi Milioni 435 zimetumika katika ujenzi wa madaraja katika barabara ya Mpetu-Matongo, Misughaa-Msule-Sambaru, Mungaa-Ntuntu-Mang’onyi na Lighwa-Ujaire na utekelezaji wake umefikia asilimia 90.

Amesema katika barabara za Misughaa-Kikio na Matongo-Mpetu kuna uhitaji wa jumla ya madaraja matatu ambayo ni Daraja la Mto Matongo lenye urefu wa mita 65, Daraja la mto Isanja lenye urefu wa mita 45, na Daraja la mto Siuyu lenye urefu wa mita 30.

Aidha,kutokana na ukubwa wa madaraja hayo usanifu wa kina unahitajika kufanywa ambapo TARURA imeanza kutekeleza kazi ya usanifu wa Madaraja haya kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi wake.

Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum Martha Gwau akiuliza kwa niaba ya Mtaturu ametaka kujua kwa kuwa Bajeti ya TARURA wilayani ni ndogo,je nini mpango wa serikali kujenga madaraja ili kukamilisha kazi nzuri inayofanyika kuunganisha barabara za vijiji na vijiji,kata na kata na hatimaye Wilaya na wilaya?

" Pia kwakuwa barabara bila madaraja haikamilki na kwakuwa tathimini ya madaraja barabara ya matongo-mpetu,Misughaa-Ntuntu,Misughaa-Kikio,Kimbwi na Ighuka imeshafanyika ni lini serikali itatenga fedha kujenga madaraja hayo?,amehoji Mbunge Gwau kwa niaba ya Mtaturu.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Katimba amesema serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba inajenga na kuboresha miundombinu maeneo yote nchini.

Amesema mtandao wa barabara nchini una kilomita 144.429 na ni mtandao mkubwa hivyo unahitaji bajeti kubwa.

"Mh Mbunge Mtaturu tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na amenieleza changamoto za miundombinu katika jimbo lake,Mh Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akichukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuongeza bajeti ya TARURA kutoka Bilioni 275 hadi Bilioni 710 mpaka sasa,"amesema Katimba.

Amemuhakikishia mbunge kuwa pale inapotokea dharura serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha mawasiliano hayakatiki na kusisisitiza dhamira ya serikali ya kufanyia kazi ujenzi wa madaraja na miundombinu yote ambayo ni muhimu kwa ajili ya wananchi.

"Niwahakikishie kuwa bajeti ya dharura imeongezwa kutoka Bilioni 21.2 hadi Bilioni 52.6,yote hii kwa sababu serikali inataka pale inapotokea dharura waweze kutatua dharura hiyo,"amesema.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/3Z6BsAh

No comments