MALAIGWANAN WAKATA SHAURI KUHAMA HIFADHI NGORONGORO
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.
Baadhi ya Wazee wa kimila (Malaigwanan) kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamekata shauri na kuamua kuondoka ndani ya hifadhi hiyo kuelekea Kijiji cha Msomera na maeneo mengine baada ya kupata elimu ya umuhimu wa kwenda kufanya shughuli nyingine ili kuboresha maisha yao na kupisha shughuli za uhifadhi.
Katika kikao maalum kilichofanyika jana usiku tarehe 10.04.2024 katika Kijiji cha Meshili kata ya Olbalbal na kuhudhuriwa na baadhi ya wazee hao wa kimila (Laigwanan) ambao wamesema kuwa wamechoka kupotoshwa kwa kupewa fedha ndogondogo ili wasiihame katika eneo hilo.
Wameongeza kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa tarafa ya Ngorongoro wamekuwa wakitoa fedha kwao ili waendelee kubaki na umaskini wakati viongozi wakubwa wanaowashawishi wasihame wengi wao wanaishi mjini Karatu na Arusha huku wao wakiishi katika maisha magumu na wengine kupoteza familia zao kwa kuliwa na wanyama.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao malaigwanan hao wamesisitiza kuwa kwa sasa wamejipanga kuondoka na tayari wapo kwenye kufuata taratibu za uandikishaji ili waweze kutoka kwenye eneo hilo na kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
“Tumechoka kudanganywa na watu ambao wamekuwa wakiishi kwa kupata fedha kutoka kwa wanasiasa na wadau wengine kupitia migongo yetu,wanatudanganya tusihame wakati wao wenyewe hawakai humu hifadhini,viongozi wetu ni wababaishaji na hawatujali zaidi ya kuendekeza matumbo yao”alisema kiongozi mmoja wa wazee hao wa kimila.
Wameongeza kuwa baadhi ya watoto wa tarafa hiyo wamegeuzwa kuwa wachungaji wa mifugo ya matajari kutokana na umaskini wa familia zao ndio maana ni kawaida hata siku za shule kukuta watoto hao wakiwa machungani badala ya kuwa shule.
Katika siku za hivi karibuni uchunguzi wa mwandishi wetu unaonesha kwamba kumekuwa na vikao vya mara kwa mara vya viongozi wa kimila ndani ya tarafa ya Ngorongoro kujadili mustakabali wao baada ya idadi kubwa ya waandishi kushawishika kuhama kutoka ndani ya hifadhi.
Viongozi hao wa kimila wamekuwa wakiziomba mamlaka zinazohusika na zoezi hilo kuwahamisha haraka kutoka ndani ya hifadhi baada ya kupata taarifa za jinsi wenzao wanavyoishi maisha mazuri,salama na yenye uhuru mkubwa katika Kijiji cha Msomera kulinganisha na maisha ndani ya hifadhi.
No comments