Breaking News

DKT. BITEKO AZITAKA TARURA,TANESCO KUFIKISHA HUDUMA ZAKE NGORONGORO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha linapeleka huduma ya umeme kwenye maeneo ya miradi ya maendeleo ili kuharahisisha huduma kwa wananchi.

Dkt. Biteko amesema hayo akiwa Loliondo, wilayani Ngorongoro baada ya kuzindua minara ya kurushia matangazo ya TBC Taifa na Bongo fm.

Amesema miradi inatekelezwa na itakuwa ya mafankio endapo Taasisi husika zitakaa pamoja na kuandaa maeneo yanayohitaji utekelezaji katika hatua mbalimbali.

  "TANESCO, REA, UCSAF na TBC  zikae pamoja wakati wa uandaaji wa miradi husika ili miradi iwe inatekelezeka kwa tija, ufanisi na kwa haraka".

Pia,  ameiagiza TARURA kuhakikisha huduma ya barabara zinafikika katika maeneo ilipojengwa mitambo ya redio ambayo ipo sehemu kubwa ya milimani nchini ili kuwa na miundombinu imara.

Pia, ameipongeza TBC kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya utangazaji, maboresho ya studio, mitambo na vifaa vya kisasa, ubora wa maudhui pamoja na ubunifu katika kuwahabarisha Watanzania.

"Mimi nafuatilia habari za TBC nafahamu chaneli ya TBC mahsusi kwa ajili kutangaza utalii (Safari Chaneli), redio ya vijana ya Bongo FM na televisheni ya vijana ya TBC2. TBC imekuwa na kampeni maalum kama vile: 27 ya Kijani kupitia Jambo Tanzania, Elimu kwa Umma kuhusu Tume ya Haki Jinai, vipindi vya kimkakati vyenye lengo la kukuza uzalendo (Mizani, jioni njema, jamvi la machweo na Lulu za Kiswahili)," amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka wananchi ambao mitambo hiyo imezinduliwa katika wilaya za Ngorongoro, Arusha, Uvinza  Kigoma, Makete - Njombe na Kyela  Mbeya, kuhakikisha wanaitunza mitambo hiyo kwa maslahi ya wananchi wote.

"Nimetaarifiwa kuwa usikivu wa redio za TBC katika kipindi cha miaka mitatu (2020/2021 – 2022/2023) ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umeongezeka kutoka asilimia 74 (2020/2021) hadi kufikia asilimia 85 (2022/2023) na utafikia asilimia 92 baada ya kukamilika miradi inayoendelea kwa Mwaka huu wa Fedha 2023/2024," amesema Dkt. Biteko.

Kuhusu uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa amewasihi watanzania kufanya  maamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo kwani Wananchi wanachotaka ni maendeleo na sio siasa.

"Tujitahidi kusikiliza vizuri sera za wagombea watakaoamua kuwania na tuamue kwa utulivu na kwa kumshirikisha Mwenye Mungu ili lengo kuu la kuwa na viongozi lifikiwe," ameongeza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amesema TBC inaendelea kuboresha miundombinu ya utangazaji ili kuwahabarisha Watanzania.

Aidha, amewataka Watanzania kusimama na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais amegusa maisha ya Watanzania kwa kuleta fedha na kujenga ncjo, kuboresha miundombinu mbalimbali hapa nchini.

No comments