DKT. BITEKO ATAKA WATANZANIA KUMUENZI SOKOINE KWA KUFANYA KAZI
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha yao.
Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kufungua Mdahalo wa Kitaifa wa Kumbukizi ya Miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.
Dkt. Biteko amesema Hayati Sokoine atakumbukwa daima kama kiongozi aliyepigania maendeleo ya taifa kwa moyo wake wote na katika uongozi wake katika nyadhifa zote alitilia mkazo wananchi kuwa ndio msingi wa maendeleo.
"Hayati Sokoine alifanya kazi kubwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya taifa na aliweka misingi imara iliyoendeleza muongozo wa kila kiongozi wa Tanzania awe wa namna gani," amesema Dkt. Biteko
Amesema, Hayati Sokoine aliwataka Viongozi wa Serikali na wananchi kueleza wamezipata mali kwa namna gani kwa hiyo watu wengi waliopata mali kwa njia haramu walimuogopa Sokoine walitupa fedha na mali nyingine kwa kuhofia kuhojiwa.
Vile vile, Dkt. Biteko amesisitiza Sekta ya Kilimo iwe kimbilio katika kuinua na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwa kuwa imeajiri watanzania wengi hususan vijana na kukipongeza chuo cha SUA kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Hayati Sokoine amefanya kazi kubwa katika maendeleo ya Sekta ya Kilimo na kuongeza kuwa Wizara ya elimu inafanya kazi kubwa kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na na mchango mkubwa kwa wananchi hususan vijana.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA, Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa, Edward Moringe Sokoine alikuwa kiongozi wa kipekee hasa katika suala la kutoa maamuzi, uzalendo, uchapa kazi, uadilifu na uaminifu.
"Kwa mfano, alifanya kazi bila kuchoka usiku na mchana, pia alisimamia sera za nchi kwa bidii na kwa weledi. Alichukia na alipiga vita ruswa na kuhakikisha nchi inapiga hatua katika maendeleo kiuchumi na kijamii," amesema Prof. Chibunda.
Mdahalo wa kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine umejadili mambo yanayohusu uongozi na mambo ambayo taifa la Tanzania limerithi kutoka kwa Sokoine ikiwemo Sokoine na Uongozi iliyowasilishwa na Mhe. Anna Makinda, Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, Uongozi na Maendeleo iliwasilishwa na Prof. Issa Shivji, Kilimo na Maendeleo iliyowasilishwa na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA na Sokoine na Maendeleo ya kilimo iliyowasilishwa na Prof. Kalunde Sibuga ambaye ni nguli wa kilimo wa chuo cha SUA.
No comments