Benki ya Biashara Tanzania yatenga bilioni 300 kwa ajili ya wajasiriamali
Benki ya TCB yalenga kuwafikia wajasiriamali 2,000
Yatangaza ongezeko la faida ya bilioni 10.7 kwa kipindi cha robo
ya kwanza Machi, 2024.
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imetenga mwaka huu 2024
imetenga shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali nchini
katika kukuza mitaji ya biashara zao.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa
Mtendaji Mkuu wa TCB Adam Mihayo wakati akizungumza na Wahariri na waandishi wa
Habari kuhusu mafanikio ya Benki hiyo.
“Mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 300 na tunapanga kuwalenga
wajasiriamali 2,000 na kwa nini nilisema hivyo, kwa sababu ni kipengere muhimu
sana ni ‘growth engine’ ya uchumi wetu, asilimia 90 ya GDP inakuwa ‘driven’ (inaendeshwa)
na hawa hapa,” alisema Mihayo na kuongeza,
“Na kwa kufanya hivyo basi, tutakuwa tunaunga mkono moja kwa
moja ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,”.
Katika hatua nyingine Mihayo alitangaza ongezeko la faida ya shilingi bilioni 10.7 za kitanzania baada ya makato ya kodi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ambayo ilifikia tamati Machi 31, 2024.
“Benki inaamini ongezeko hili la asilimia 358 katika mapato
yake kipindi cha robo ya kwanza yametokana na ukuaji mkubwa wa mapato katika
aina zake zote za biashara na ongezeko kubwa la kitabu cha mizania katika
kipindi tajwa kilichopitiwa,” alisema Mihayo.
Mihayo alieleza kuwa mapato yaliongezeka kwa asilimia 30
mpaka kufikia shilingi bilioni 56.8 za kitanzania yakiimarishwa na kitabu cha
mizania na kasi kubwa ya ukuaji katika mapato yote.
Aidha, alisema amana za wateja zimeongezeka kwa asilimia 12
kufikia shilingi trilioni 1.1 za kitanzania ikiashiria imani kubwa ya wateja kwa
benki, wakati huohuo mikopo kwa wateja imepanda kwa asilimia 15.4 kufikia
shilingi bilioni 983.6 za kitanzania hadi Machi 31, 2024.
Kwamba hiyo inaonyesha dhamira ya benki katika kuwezesha
ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu wake.
Alisema, “Ninajivunia kuwatangazia utendaji wetu wa kipekee
katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024. Ukuaji mkubwa huu unasukumwa
na dhamira yetu ya dhati na kujizatiti kwetu katika ufanisi ili kumridhisha
mteja. Sisi ni benki ambayo inachukua muda wake kuwasikiliza wateja wetu na
kuweka juhudi katika kuelewa mahitaji yao.”
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Adam Mihayo katika mkutano unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina mkutano huo uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Aliendelea kusema, “kwa ongezeko hili la mapato kwa asilimia
30 tumedhihirisha kwa mara nyingine tena ujasiri wetu, na uwezo wetu wa
kulikabili soko linalokua kwa kasi. Imani ya wateja wetu kwetu bado ni imara
kama inavyothibitishwa na ongezeko la amana ya wateja. Vile vile, dhamira yetu
katika kuimarisha ukuaji wa Uchumi inadhihirika wazi katika ongezeko la mikopo
kwa wateja wetu. Tukiendelea na safari hii ya mafanikio, tunajizatiti
kuwafikishia watu ubunifu wa kifedha na kuchangia katika ustawi wa watu wetu na
Taifa letu kwa ujumla.”
Alieleza jumla ya gharama kulingana na kipato katika robo hii
ya kwanza ni shilingi bilioni 43.2 za kitanzania, sawa na ongezeko la asilimia
6.1 ukilinganisha shilingi bilioni 40.7 na robo ya kwanza ya mwaka jana 2023,
wakati huohuo jumla ya gharama za uendeshaji imepanda kidogo kutoka shilingi
bilioni 26.5 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi
kufikia shilingi bilioni 26.8 za kitanzania mwishoni mwa robo ya kwanza ya
mwaka 2024.
Mkurugenzi Mtendaji TCB, Adam Mihayo alisisitiza kuwa, “tumejizatiti
kuendeleza jitihada katika kutekeleza mkakati wetu ambao unazingatia ufanisi wa
uendeshaji, na kuendelea kupunguza gharama zetu kwa uwiano wa mapato licha ya
kuongezeka kwa kipindi hiki."
Aliongeza, Benki inahusisha ukuaji huu wa faida na maendeleo
endelevu ya biashara ndogondogo na za kati nchini. Hali kadhalika, katika
kufikia lengo la benki juu ya wafanyabiashara wadogowadogo na wakati, TCB Benki
imetumia njia ya kidigitali katika kufanya ufumbuzi wa kibenki, na hivyo kuwapa
wateja wake ufanisi, urahisi na uwezo wa kufanya shughuli za kimiamala.
Kwamba mwelekeo huu wa kimkakati unaimarishwa na mkakati wa
kidigitali unaoendelea, ambao umeiwezesha benki kuwa karibu zaidi na wateja
wake kuliko awali na kuwaruhusu wao kuendelea kujipatia huduma za kibenki
katika sehemu zinazowapendeza wao na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya benki
na wateja wake.
Alibainishwa kwamba, mtandao wa mawakala wa kibenki wa TCB
Benki, umekua kwa takribani mara nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,
kutoka idadi ya mawakala 1,584 mwaka 2020 hadi zaidi ya mawakala 6,000 kwa
mwaka 2023.
Alibainisha, idadi ya mashine za UmojaSwitch za ATM
zimeongezeka kutoka 250 mwaka 2020 hadi kufikia mashine 281 kwa mwaka 2023.
Katika kipindi hiki, TCB Benki pia imeanza kutoa kadi za VISA.
Alieleza UmojaSwitch imeingia ubia na NMB Benki na katika
robo hii ya kwanza ya mwaka 2024, kwamba tayari kuna mashine za ATM 750 za NMB ambazo
zimeunganishwa na ATM za UmojaSwitch.
“Hii inafanya jumla ya mashine za ATM za UmojaSwitch kufikia
1,031 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024. TCB Benki imeweza kuanzisha bidhaa
bora kama vile, M-Koba. Nimatumaini ya uongozi kwamba tutaendelea kutoa bidhaa zinazowalenga
wateja ambazo zitaendelea kuvunja rekodi kwa kipindi chote cha mwaka 2024 na
kuendelea,”.
No comments