Breaking News

Serikali kupitia TBS hutenga zaidi ya milioni 250 kuhudumia wajasiriamali.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mafanikio na Majukumu ya Shirika hilo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano na Wahariri na waandishi wa Habari, kilichofanyika leo Aprili 15,2024, Jijini Dar es Salaam, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

*Yatoa leseni za ubora wa bidhaa 2,106 kwa kipindi cha miaka mitatu

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imekuwa ikitenga zaidi ya shilingi milioni 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Athumany Ngenya akizungumza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji, majukumu na mafanikio ya Shirika hilo.

Kuhusu utoaji wa leseni za Alama ya Ubora, Dkt. Ngenya alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.

“Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa Wajasiriamali wadogo. Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa  viliandaliwa sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango hivyo viliandaliwa katika Nyanja mbalimbali,” alisema Dkt. Ngenya.

Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabatho Kosuri, akizungumza alipokuwa akitoa neno la utangulizi katika mkutano huo.

Kwamba TBS imeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara vya Afrika Mashariki na Afrika nzima.

Akizungumzia kuhusu mafunzo kwa Wazalishaji na Wajasiriamali Dkt. Ngenya alibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya wadau 5,789 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo hayo.

Kwamba TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Dkt. Ngenya alisema katika ukaguzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini, Shirika limeandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote hapa nchini ili kuhakikisha kwamba vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

Hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.

Alisema, TBS katika utekelezaji wa majukumu yake imepata mafanikio kadhaa ikiwemo ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga Maabara katika Mikoa ya  kimkakati

Kwamba Shirika linatekeleza mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Shirika na maabara (Viwango House-Dodoma) ambapo Maabara hii itahudumia mikoa mitatu (3) ya kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu.

Dkt. Ngenya alibainisha kuwa, Shirika linatarajia kuanza ujenzi wa maabara yakisasa katika kanda ya Ziwa (Mwanza) na kanda ya kaskazini (Arusha) huku Maabara ya kanda ya ziwa ikitarajiwa kuhudumia mikoa sita (6) ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

 Wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari na waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mafanikio na Majukumu ya Shirika hilo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan , kilichofanyika leo Aprili 15,2024, Jijini Dar es Salaam, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Aliendelea kueleza, Maabara ya kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne (4) ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.

Mafanikio mengine ni kuongeza na kuimarisha ofisi za kanda, kwamba Shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha) ,Kanda ya Kusini (Mtwara) ,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya ziwa (Mwanza), Kanda ya Kati (Dodoma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).

Kwamba Kanda hizi zina ofisi katika mipaka, bandari pamoja na viwanja vya ndege.

Kadhalika alisema TBS imefanikiwa kuongeza ufanisi katika utoaji huduma ikiwemo ununuzi wa mashine za kisasa za maabara.

Alifafanua kuwa, Shirika limewekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya maabara vya kisasa (state-of-the-art-equipment) kwa kutumia fedha za ndani pamoja na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Kuhusu, ithibati za umahiri katika maabara, alisema Shirika lina maabara 12 zilizopo Ubungo Dar es Salaam, maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa kimataifa (accreditation).

Alisema hatua hiyo inapelekea majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo kuaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara.

 \

No comments