KAMATI YA BUNGE KUKAGUA MIRADI MITANO YA OWM-KVAU
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inatarajia kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mitano inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu (OWM-KVAU) na taasisi zilizo chini yake.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, Machinjio ya kisasa Nguru Hills, ukarabati wa kiwanda cha chai Mponde, kukagua Chuo cha Ufundi kwa Watu wenye Ulemavu cha Masiwani na kukagua ujenzi wa vitalu nyumba mkoani Arusha.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako aliokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo itakayotembelewa na kamati.
Prof.Ndalichako amesema ratiba ya shughuli za kamati inaonesha kamati hiyo kutembelea na kukagua miradi hiyo ambapo kwa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi(shamba la mbigiri) unaomilikiwa na mfuko wa NSSF kwa asilimia 96 umefikia asilimia 89 na uzalishaji unatarajiwa kuanza Julai mwaka 2023.
Aidha, amesema mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro unaomilikiwa na mfuko wa PSSSF kwa asilimia 39 utazalisha ajira za moja kwa moja zisizopungua 350 na zaidi ya ajira 2,000 zitakazotokana na mnyororo wa thamani.
Amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1,000 kwa siku na kampuni ya Nguru itanunua mifugo hiyo moja kwa moja kwa wafugaji wa kibiashara wenye mifugo yenye kiwango kinacholingana na mahitaji ya kiwanda.
Kuhusu kiwanda cha chai Mponde, Prof.Ndalichako amesema tayari kimeanza kufanya kazi na kilo 24,460 zimeuzwa na tani 50 zinategemewa kuuzwa mwishoni mwa mwezi Machi, 2023.
Akizungumzia Chuo cha Masiwani, Mhe. Waziri Ndalichako amesema ni miongoni mwa vyuo sita vilivyo chini ya ofisi hiyo kinachotoa elimu ya uzalishaji mali na kinamsaidia mtu mwenye ulemavu kwa kumfundisha mbinu za marekebisho ya viungo ili kumuwezesha kufanya kazi mbalimbali.
Kadhalika, amesema katika ujenzi wa vitalu nyumba upo chini ya programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi na vijana 12,580 kutoka Halmashauri 117 za Mikoa 17 nchini wamenufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.
Ameahidi Ofisi hiyo itaipa kamati hiyo ushirikiano ili kuishauri serikali masuala mbalimbali ya utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq amepongeza Ofisi hiyo kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kushirikiana ili kutoa ushauri kwa serikali utakaoleta tija zaidi kwa Ofisi hiyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof.Jamal Katundu, amesema Ofisi hiyo ndio yenye jukumu la kuratibu fursa za ajira ili kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 iliyoahidi ajira milioni nane zitengenezwe kwa kipindi hicho.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/8T4qFJo
No comments